SUSAN KING'ORI: Napenda kufanya kazi na Maria wa Citizen TV
Na JOHN KIMWERE
‘MTAKA cha mvunguni sharti ainame.’ Ndivyo wahenga walivyosema na tangia zama hizo ndivyo ilivyo hadi sasa. Ni msemo ambao kwa muda unaendelea kuonekana una mashiko sio haba miongoni mwa jamii.
Pia unaonekana unaendelea kudhihirishwa na wana dada wengi tu hasa wale wameamua kujituma kisabuni kwenye masuala mbali mbali katika harakati za kujitafutia riziki.
Kati yao ni binti, Susan Gathoni King’ori mwigizaji anayekuja pia mwanafunzi wa kidato cha nne kwenye shule ya Nembu Girls. Katika mpango mzima msichana huyu aliyezaliwa mwaka 2003 anasema anadhamiria kuhitimu kwa taaluma ya uigizaji.
”Nilianza kushiriki michezo ya kuigiza kanisani nikiwa mdogo ambapo ninalenga kuibuka miongoni mwa waigizaji sifika duniani miaka ijayo,” alisema na kuongeza kwamba kando na hayo anashiriki uigizaji baada ya kuvutiwa na filamu iitwayo ‘Shuga’ ya msanii Lupita Nyong’o mzawa wa Kenya anayetamba kwenye filamu za Hoollywood.
Kando na Lupita msichana huyu anasema anashiriki maigizo akilenga kufikia upeo wa mwigizaji mahiri mzawa wa Marekani, Tyler Perry. Msanii huyo anajivunia kushiriki filamu kama ‘Oval,’ ‘A madea Family Fune,’ ‘A fall from Grace,’ ‘ Nobody’s Fool,’ ‘The Single Moms Club,’ ‘Gone girl,’ ‘Good Deeds,’ na ‘Alex Cross,’ kati ya zinginezo.
Ndio mwanzo ameanza kupiga ngoma katika masuala ya filamu ambapo alishiriki filamu ya kwanza mwaka uliyopita kwa jina ‘Mpango wa Kando,’ chini ya Vuma productions. Brandi hiyo inamilikiwa na mwigizaji anayekuja Princess Zuena Abdallah maarufu kama First Princess, Zawadi pia Nalubega.
”Msanii yeyote hufanya kazi yake akitarajia kufanya vizuri hivyo tunaamini filamu hiyo itafanya kweli katika tasnia ya maigizo,” alisema na kutoa mwito kwa Wakenya kuwapa sapoti wasanii wa humu nchini. Anadokeza kuwa vyombo vya habari vimechangia Wakenya wengi kutowapa sapoti kwa kupuuza kazi za wazalendo.
”Kiukweli vyombo vya habari vinastahili kuzipatia kazi za wazalendo kipau mbele badala ya kupeperusha filamu za waigizaji wa kigeni,” akasema.
Msichana huyu anasema hapa nchini angependa sana kufanya kazi na wasanii kama Catherine Kamau (Selina) na Yasmin Said (Maria) waigizaji kwenye filamu za Selina na Maria mtawalia.
Kisura huyu anawaponda Wakenya ambao hupenda kupuuza filamu za Wazalendo na kuwanyima nafasi ya kusonga mbele.
Anasema Wakenya wanastahili kuwa mstari wa kwanza kuziunga mkono kazi za wenzao kinyume na mtindo wao ambapo wanapenda kutazama filamu za kigeni.
Licha ya kuwa hajakomaa katika maigizo sio mchoyo wa mawaidha, anahimiza wanadada wanaoibukia kujipa moyo na kujiamini wanaweza pia kumweka Mungu mbele kwa yote wanayofanya.
Anasema Wakenya wanaweza kufanya vizuri zaidi sawia na wenzao katika mataifa kama Nigeria, Tanzania na Afrika Kusini kati ya mengineo.