Michezo

'YouTube Man' alenga kufufua makali yake Diamond League Qatar

May 2nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA wa dunia mwaka 2015 Julius ‘YouTube Man’ Yego atajaribu kufufua taaluma yake ya kurusha mkuki katika duru ya kufungua msiamu wa Riadha za Diamond League nchini Qatar hapo Mei 4, 2018. 

Yego, ambaye alishinda taji la Jumuiya ya Madola mwaka 2014 na Bara Afrika mwaka 2012 na 2014, amekuwa akisikitisha miaka ya hivi karibuni.

Mshikilizi huyu wa rekodi ya Afrika ya mtupo wa mita 92.72 aliyoweka akishinda taji la dunia jijini Beijing nchini Uchina mwaka 2015, alikuwa mjini Gold Coast nchini Australia mwezi uliopita wa Aprili kwa michezo ya Jumuiya ya Madola.

Mwanariadha huyu mwenye umri wa miaka 29 alisikitisha alipobanduliwa nje katika raundi ya kwanza baada ya kurusha mkuki umbali wa mita 74.55, mtupo wake mzuri mwaka 2018.

Mtupo wa Yego bora mwaka 2017 ulikuwa 87.97 ambao alipata jijini Nairobi katika mashindano ya kufuzu kushiriki Riadha za Dunia jijini London nchini Uingereza.

Alifika fainali jijini London akiwa na mtupo wa mita 83.57, lakini akarusha mkuki umbali wa mita 76.29 katika fainali hiyo na kumaliza katika nafasi ya 13.

Yego atakabiliana na warushaji wengine tisa wa mkuki wakiwemo Johannes Vetter (Ujerumani) na raia wa Jamhuri ya Czech Jakub Vadlejch na Petr Frydrych ambao walishinda medali za dhahabu, fedha na shaba katika Riadha za Dunia mwaka 2017.

Bingwa wa Olimpiki Thomas Rohler kutoka Ujerumani pia yuko katika orodha ya washiriki.