Habari

BBI: Wahudumu wa afya washinikiza tume ya huduma za afya iundwe

June 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WAHUDUMU wa afya wameendeleza kampeni ya kushinikiza pendekezo la kuundwa kwa Tume ya Huduma za Afya (Health Service Commission-HSC) lijumuishwe katika ripoti ya mwisho ya mpango wa maridhiano (BBI) itakayotolewa wiki ijayo.

Wawakilishi vyama vya kutetea masilahi ya madaktari, maafisa wa kliniki, wauguzi, wataalamu wa maabara na wahudumu wengine wameonya kuwa wanachana wao watavuruga kabisa shughuli katika hospitali zote nchini ikiwa pendekezo la kuundwa kwa tume hiyo halijumuishwi kwenye mswada wa marekebisho ya Katiba.

“Tungependa kutangaza hapo leo kwamba mipango inayoendesha na watu fulani wa kuondoa pendekezo la kuundwa kwa HSC kwenye ripoti ya BBI ikome. Ikiwa watathubutu kuondoa pendekezo hili kutoka ripoti ya BBI tutafunga hospitali zote nchini,” akasema Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wauguzi (KNUN) Seth Panyako.

Alisema pendekezo hilo lilikuwa kwenye ripoti ya kwanza ya BBI ambayo ilizinduliwa mnamo Novemba 17, 2019 na halipasi kuondolewa.

“Wadau wote katika sekta ya afya waliowasilisha maoni yao mbele ya jopokazi la BBI walitaka kuundwa kwa tume kama hii ambayo itasimamia masuala yanayohusiana na masilahi ya wahudumu wa afya kama vile ulipaji mishahara na kupandishwa vyeo kwa maafisa mbalimbali,” Bw Panyako akasema Jumatano jioni kwenye kikao na wanahabari katika Railways Club, Nairobi.

Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa wa Kliniki Peterson Wachira alisema ni aibu kwamba wahudumu wa afya nchini nyakati nyingi hugoma sababu ikiwa ni kucheleweshwa kwa mishahara yao, ilhali sheria inasema kuwa sharti mfanyakazi yeyote alipwe mshahara wake kila mwisho wa mwezi.

Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa wa Kliniki Peterson Wachira. Picha/ Charles Wasonga

“Hatujawahi kusikia watumishi wa umma, maafisa wa idara ya mahakama au walimu wakigoma kwa kutolipwa mishahara kwa wakati. Hii ni kwa sababu wafanyakazi hawa wanayo tume mahsusi ya kusimamia suala kama hili,” akasema Bw Wachira.

Wafanyakazi wa umma wanasimamiwa na Tume ya Utumishi wa Umma (PSC), wale wa Idara ya Mahakama wako chini ya Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) huku masilahi ya walimu wakiendeshwa na Tume ya Huduma za Walimu.

Tume hizi tatu ni miongoni mwa tume ambazo zimebuniwa na Katiba ya sasa ambayo ilizinduliwa mnamo Agosti 27, 2010.

Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari, Wataalamu wa Dawa na Madaktari wa Meno Nchini (KMPDU) Hamisi Mwachonda alielekeza kidole cha lawama kwa magavana ambao alisema wanavuruga sekta hiyo ya afya kwa kutotilia maanani masilahi ya wahudumu wa afya.

“Hii ndio maana wakati huu wakati huu wahudumu wa afya wamegoma katika kaunti ya Kisumu ihali wenzetu katika kaunti za Nandi, Kisii na Mambasa wametoa ilani ya kugoma kuanzia mwezi ujao. Wakati kama huu wahudumu wa afya hawafai kugoma kwa sababu huduma zao zinahitajika zaidi katika mchakato mzima za kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19,” akasema Dkt Mwachonda.

Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari, Wataalamu wa Dawa na Madaktari wa Meno Nchini (KMPDU) Hamisi Mwachonda. Picha/ Charles Wasonga

Viongozi hao wa vyama vya wahudumu wa afya walizilaumu serikali za kaunti kwa kuendeleza ukabila na mapendeleo wakati wa kuajiriwa wahudumu wa afya na hata shughuli ya kuwapandisha vyeo.

“Hii ndio maana baadhi ya wahudumu wa afya hawajahitimu inavyohitajika, hali ambayo huhatarisha maisha ya wagonjwa. Hali kama hii haiwezi kutokea ikiwa kutakuwepo na Tume ya Huduma za Afya itakayotwika wajibu wa kusimamia shughuli zima la kuajiri wahudumu wa afya. Kazi kama hii haipasi kuachwa mikononi mwa magavana, ambao ni wanasiasa,” akasema Bw Wachira.