• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Ni rasmi Liverpool ndio mabingwa wa EPL

Ni rasmi Liverpool ndio mabingwa wa EPL

Na CHRIS ADUNGO

LIVERPOOL walinyakua ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 mnamo Juni 25 kufuatia ushindi wa 2-1 uliosajiliwa na Chelsea dhidi ya mabingwa watetezi Manchester City.

Ushindi kwa Man-City uwanjani Stamford Bridge ungalichelewesha zaidi karamu ya Liverpool wanaotiwa makali na kocha mzawa wa Ujerumani, Jurgen Klopp.

Katika kipindi cha misimu miwili iliyopita ya EPL, Man-City walikuwa wamepoteza jumla ya michuano sita pekee na kutawazwa wafalme wa 2017-18 na 2018-19 kwa alama 100 na 98 mtawalia.

Ingawa hivyo, kichapo kutoka kwa Chelsea, ambacho kilikuwa chao cha nane kupokea msimu huu, kiliwasaza na alama 23 zaidi nyuma ya Liverpool.

Liverpool walitwaa rasmi ubingwa wa soka ya Uingereza msimu huu zikisalia mechi saba zaidi katika kampeni za kivumbi hicho.

Fowadi Christian Pulisic ambaye ni mzawa wa Amerika, aliwaweka Chelsea kifua mbele kunako dakika ya 36 kabla ya juhudi zake kufutwa na kiungo matata wa Ubelgiji, Kevin De Bruyne aliyesawazishia Man-City katika dakika ya 55.

Liverpool walithibitishiwa ufalme wa EPL kunako dakika ya 78 baada ya kiungo Fernandinho kuunawa mpira ndani ya kijisanduku chao na kuwapa Chelsea penalti iliyofumwa wavuni na Willian.

Ushindi huo wa Chelsea unamaanisha kwamba Man-City kwa sasa watalazimika kuandalia Liverpool gwaride la heshima watakapokutana kwa gozi jingine la EPL uwanjani Etihad mnamo Alhamisi ya Julai 2, 2020.

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City wangali na matumaini hai ya kujitwalia jumla ya mataji mawili zaidi katika kampeni za msimu huu. Baada ya kuhifadhi ubingwa wa League Cup, Man-City wamo katika robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na robo-fainali za Kombe la FA ambapo watavaana na Newcastle United mnamo Juni 28, 2020 uwanjani St James’ Park.

Subira ya Liverpool ya kutwaa taji la 19 la EPL ilirefushwa zaidi na likizo ya miezi mitatu iliyosababishwa na janga la corona lililositisha kampeni za msimu huu mnamo Machi 13, 2020. Kipute hicho kilirejelewa mnamo Juni 17, 2020.

You can share this post!

Dortmund wamsajili beki matata Thomas Meunier kutoka PSG

Mutyambai aamuru kukamatwa kwa afisa aliyempiga risasi...

adminleo