• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
Kamati ya kitaifa ya Olimpiki kuwapa wanariadha wastaafu msaada wa chakula na pesa

Kamati ya kitaifa ya Olimpiki kuwapa wanariadha wastaafu msaada wa chakula na pesa

Na CHRIS ADUNGO

KAMATI ya Kitaifa ya Olimpiki (NOC-K) imeanza kutekeleza mpango wa kutoa msaada wa vyakula na pesa kwa wanariadha wastaafu waliowahi kuwakilisha Kenya katika mashindano mbalimbali ya kimataifa enzi zao.

Wanaonufaika na mpango huo ni wanariadha wazawa wa Kenya waliowahi kunogesha michezo ya Olimpiki, Jumuiya ya Madola na ile ya bara la Afrika kabla ya kustaafu kufikia mwisho wa 2004.

Mradi wa kuwapa msaada wanariadha hao ulianzishwa mnamo Mei 2020 kwa kiasi cha Sh500,000 kutoka kwa NOC-K.

Kwa mujibu wa Francis Mutuku ambaye ni kaimu katibu mkuu wa NOC-K, jumla ya wanariadha 89 waliopeperusha bendera ya Kenya katika majukwaa mbalimbali wamekwisha tambuliwa na wataanza kunufaika kutokana na mpango huo kwa kupokeza vyakula vya thamani ya Sh2,000 na Sh500 za matumizi kwa kipindi cha miezi mitatu ijayo.

Kulingana naye, janga la Covid-19 limesitisha shughuli nyingi za michezo; suala lililowaweka katika ulazima wa kuanza kufikiria upya jinsi ya kuwasaidia wanariadha wa zamani katika kipindi hiki kigumu.

“Tumeona haja ya kuwatilia shime mashujaa wetu. Mpango wetu ni kupanua zaidi orodha ya watakaonufaika na kuongeza kipato tunachotoa kwa minajili ya kuwafaa. Hata hivyo, tumeanza na kidogo tulicho nacho,” akaongeza Mutuku.

“Kutokana na uchache wa rasilmali, tumewalenga kwanza maveterani waliowakilisha Kenya katika mashindnao ya Olimpiki, Jumuiya ya Madola na michezo ya bara la Afrika. Tutawafikia wengine pindi tutakapopata wahisani na washirika watakaozipiga jeki juhudi zetu,” akasisitiza.

You can share this post!

COVID-19: Serikali kuwalinda wauguzi

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Aina za wahusika

adminleo