Aliyeingia Ikulu akitaka kushauriana na Uhuru kuhusu ibada aachiliwa
Na RICHARD MUNGUTI
MAHAKAMA ya Milimani imemwachilia huru mwanamume aliyeingia Ikulu ya Nairobi akidai anataka kushauriana na kujadiliana na Rais Uhuru Kenyatta jinsi ya kutekeleza ibada kupata thawabu kutoka kwa Allah.
Hakimu mwandamizi Bw Daniel Ndungi alimkabidi Luqman Ali Mahmmoud kwa mjomba wake Bw Saudi Abdallah ampeleke hospitali kutibiwa maradhi ya akili.
Na wakati huo huo Bw Ndungi alimuonya Bw Abdallah kwamba atashtakiwa kortini endapo atamwachilia Luqman kurudi Ikulu ya Nairobi mara nyingine.
“Utakamatwa na kushtakiwa endapo utamwachilia Luqman kurudi Ikulu ya Nairobi akitaka kushauriana na Rais Kenyatta masuala ya ibada kwa Allah,” Bw Ndungi alimtahadharisha Bw Abdallah.
Mahakama ilimwagiza Luqman ashirikiane na mjomba wake apate tiba ya maradhi ya ubongo anayougua.
Bw Ndungi alimwachilia mshtakiwa chini ya kifungu cha sheria nambari 87(a) cha sheria za uhalifu.
Alimtahadharisha mshtakiwa kwamba “endapo atathubutu kurudi Ikulu ya Nairobi tena akisingizia anataka kufanya mashauriano na Rais Kenyatta atakiona cha mtema kuni kwa vile atafikishwa kortini tena na kuadhibiwa vikali.”
“Umeelewa vile nimekueleza?” Bw Ndungi alimwuliza mshtakiwa.
Luqman akajibu.
“Ndio nimeelewa kabisa. Sitarudi Ikulu ya Nairobi tena,” Luqman alimhakikishia hakimu.
“Basi mahakama imekukabidhi kwa Bw Abdalla baada ya upande wa mashtaka kutamatisha kesi hii inayokukabili,” Bw Ndungi alimweleza mshtakiwa.
Hakimu alimwachilia mshtakiwa baada ya kukabidhiwa ripoti kutoka kwa hospitali ya kutibu maradhi ya ubongo iliyosema: “Luqman amekuwa akiugua maradhi ya ubongo kwa muda mrefu.”
Bw Ndungi alisema mjomba aliomba korti imruhusu amchukue Luqman ampeleke hospitalini na kukaa chini ya ulinzi na uangalizi wake.
“Hii mahakama haiwezi kukataa ombi la Bw Abdallah,” alisema hakimu.
Luqman alitiwa nguvuni baada ya kukaidi agizo la maafisa watatu wa polisi wakitaka asimame afanyiwe ukaguzi kabla ya kuingilia lango nambari D.
Maafisa waliomsimamisha Luqman ni Konstebo Duncan Orero, Konstebo Winston Abwawo na Koplo Alex Sirongo.
Mshtakiwa aliyekuwa akiendesha gari aina ya Volkswagen Polo nambari ya usajili KCP 048Y aliingia Ikulu mwendo wa saa kumi na nusu kwa nguvu.
Hakimu alielezwa ilibidi polisi wapige risasi magurudumu ya gari alilokuwa anaendesha mshtakiwa ndipo lisimame.
Luqman pia alikabiliwa na shtaka la kuingia pahala pasiporuhusiwa umma kuingia.
Mnamo Juni 19, 2020, Luqman alishtakiwa kwamba aliingia Ikulu ya Nairobi ambapo mmoja hawezi kuingia bila idhini.
Mshtakiwa alikiri shtaka dhidi yake huku akieleza korti lengo lake kuingia Ikulu lilikuwa kushauriana na kuelewana na Rais Kenyatta kuhusu masuala ya utekelezaji ibada kwa Allah.”