• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:07 PM
Vikundi 45 Thika vyapokea Sh4.8 milioni za Uwezo

Vikundi 45 Thika vyapokea Sh4.8 milioni za Uwezo

Na LAWRENCE ONGARO

VIKUNDI 45 vya biashara vimenufaika na fedha za Uwezo Sh4.8 milioni zitakazowasaidia kupiga jeki biashara zao.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina, amewashauri wanufaika wawe na maono wanapopokea fedha hizo.

“Ninawahimiza muwe watu wanaolenga mbele ili kufanikiwa katika biashara zenu. Fedha hizo mnazopokea sio za kujifurahisha bali ni za kuendeleza biashara zenu,” alisema Bw Wainaina.

Kila kikundi kinapokea Sh100,000 ambapo kimoja huwaleta pamoja watu 10 wanaoendesha biashara.

Aliyasema hayo katika shule ya msingi ya Mugumo-ini iliyoko mjini Thika wakati wa kuwakabidhi wafanyabiashara hundi zao.

Bi Susan Wambui Ngure anasema fedha hizo za Uwezo ni muhimu sana kwao kwa sababu zitainua biashara zao.

“Kila mmoja wetu katika kikundi hujishughulisha na ,ambo kama uuzaji matunda, nguo za watoto, kufuga kuku, na hata kuuza maharage na vyakula vinginevyo,” akasema Bi Ngure.

Aliwahimiza watu wanaotaka kujiendeleza kimaisha kuzingatia mikopo wa hazina ya Uwezo ili kupiga hatua.

Bi Julia Kiongo ambaye pia ni mfanyabiashara alipongeza juhudi za mbunge wa Thika Bw Wainaina kwa kuwapa nafasi wafanyabiashara kujinufaisha na fedha za Uwezo.

Bw Wainaina aliwahimiza wananchi kuzingatia masharti ya serikali ya kupambana na maradhi ya Covid-19.

“Wakati huu tunapokabiliana na homa ya corona, kila Mkenya anastahili kujikinga ili kuzuia maambukizi zaidi,” akasema.

Alibainisha cha muhimu zaidi kwa sasa ni kuvamia barakoa, huku watu wakizingatia kuweka nafasi ya mita moja kutoka kwa mmoja hadi kwa mwingine. Baadaye kunawa mikono nako ni muhimu.

Aliwashauri wananchi wasiwe na tabia ya kutembea kwa jamaa na marafiki zao.

“Wakati huu tunapopambana na Covid-19 kila mmoja anastahili kusalia kwake nyumbani, huku tukiwa mstari wa mbele kuwahamasisha watoto wetu kuhusu janga hilo,” alisema Bw Wainaina.

Aliipongeza serikali akisema Rais Uhuru Kenyatta amejaribu kudhibiti hali hiyo kwa kuweka kafyu, na kuzuia usafiri wa kuingia na kutoka katika kaunti kama Nairobi, Mombasa, Kilifi, na hata Kwale.

Alitoa mwito kwa kila mmoja kuwa mstari wa mbele kukabiliana na janga hili la corona ili “tuweze kufungua biashara zetu kwa pamoja.”

Hafla hiyo iliyohudhuriwa na watu wachache ilichukua muda mfupi wa saa moja pekee ili kufuata maagizo muhimu ya serikali kukabiliana na homa ya Covid-19.

Mbunge huyo aliandamana na kamishna wa Thika Magharibi Bw Douglas Mutai ambaye alipongeza juhudi za mbunge huyo kuwa mstari wa mbele kwa kuipeleka Thika mbele kimaendeleo.

You can share this post!

Aliyeingia Ikulu akitaka kushauriana na Uhuru kuhusu ibada...

Wakenya wanaendelea kufurahia uhuru wa kutembea jioni baada...

adminleo