Makala

UMBEA: Mke, elewa nafasi yako katika ndoa sio kujibeba kama bendera

June 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SIZARINA HAMISI

MKE mwenye busara huelewa mipaka. Mipaka hii inahusu wajibu kama mke, wajibu kama mama iwapo umejaliwa watoto na mipaka ya ndugu, jamaa na marafiki.

Mipaka ya mke katika uhusiano na mumewe inahusu zaidi wajibu wake katika ndoa. Kwani wapo akina dada wavivu kupindukia, mwanamke kama huyu anathubutu kuuchapa usingizi na kumuachia majukumu yote msichana wa kazi.

Mumewe anapoamka kwenda kazini ama kwenye majukumu yake yeye atabaki amelala baada ya kumuagiza msichana wa kazi apike chai na atayarishe nguo za mumewe.

Kwamba hata mumewe anapoondoka asubuhi, yeye hana habari amevalia nguo gani, hajui amependeza au haikumpendeza.

Ataendelea kuuchapa usingizi na akiamka saa nne asubuhi, chumba kichafu na jambo la kwanza ni kuchukua simu na kuingia kwenye mtandao kuangalia umbea wa siku hiyo. Na bado unajiita mke dadangu?

Kuongeza chumvi kwenye kidonda, unakuta dada huyu anazaa watoto kama kuku wa kienyeji. Hajali wala kuangalia hali halisi na maisha yaliyopo nyumbani kwake na huenda maisha yao ni ya kuhangaika lakini hachukui hatua ya kuhakikisha watoto wanapatikana kwa mpangilio.

Unakutana na mwanamke ana watoto saba lakini wanaishi chumba kimoja.

Nalisema hili baada ya kushuhudia dada mmoja akisumbuka na watoto wanne ambao wamepishana kwa miezi na si mwaka. Nami kama kawaida huwa napenda kudodosa. Nikamwuliza sababu ya kuzaa watoto kama mayai ya chura. Alichoniambia nilichoka, nikaamini kama akiendelea vile basi atajaza timu ya mpira na wachezaji wa akiba.

Alinieleza kuwa mumewe ni askari na kuna kipindi kutokana na kazi yake, huwa anarudi nyumbani muda usio maalum.

Yeye akaamini mumewe ana mwanamke wa nje, kwa vile haki yake ya ndoa kuipata imekuwa patashika. Kwa hiyo siku akipatikana kutoa huduma kwa mkewe, yeye huwa hajali wala kuangalia iwapo siku hiyo anaweza kushika mimba, anamkaba mumewe hadi apate haki yake.

Hii tabia ikasababisha kila akikutana na mumewe anaruka na ujauzito kitu ambacho hakimpi taabu kwa vile anaamini hana njia nyingine ya kupata haki yake kwa mumewe.

Kwa upande mwingine iwapo kaka nawe uko kwenye ndoa, shiriki kwenye kupanga idadi ya watoto mnaoweza kuwamudu.

Hakuna ufahari wowote kumzalisha mkeo kama kuku wa kienyeji.

Halikadhalika mkeo hukumuoa kumuweka mapambo nyumbani kwako. Anahitaji huduma muhimu kutoka kwako hivyo usimnyime ama kumuwekea udhibiti wa hiyo huduma.

Unamnyima haki yake, akaipate wapi au unataka kumlazimisha achepuke nje ya ndoa ili upate sababu ya kumtelekezea mtoto?

Hivyo dada, nazungumzia mipaka kama mke. Elewa nafasi yako katika kuleta maendeleo na ufanisi katika ndoa yako. Jambo unalotakiwa kutambua ni kuwa wapo wanawake wengi tena wazuri, na wanaojipamba ili kuwanasa waume za watu.