Madiwani sitisheni wimbi la kuwaondoa magavana, Oparanya arai
Na CHARLES WASONGA
MWENYEKITI wa Baraza la Magavana (CoG) ambaye pia ni Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa wamewataka madiwani kote nchini kusitisha mtindo wa kuwasilisha hoja za kuwaondoa magavana ofisini bali wapige jeki vita dhidi ya Covid-19.
Akiongea na wanahabari jijini Nairobi Jumatatu, Oparanya amewakumbusha madiwani hao kuwa kaunti nyingi hazijaweka mikakati ya kukabiliana na kuenea kwa virusi vya corona na akawataka kuelekeza nguvu zao katika juhudi za kupambana na janga hilo.
“Tunawaomba madiwani kwamba hizi pesa wanazotumia kuwalipa mawakili kuwasaidia kufanikisha hoja za kuwaondoa mamlakani magavana zitumika katika ununuzi wa vifaa vya kujikinga na kupanuliwa kwa vituo vya kuwashughulikia wagonjwa wa Covid-19,” Bw Oparanya akasema akifichua kaunti zinakumbwa na uhaba wa fedha.
Akaongeza: “Tayari tumeomba Rais Uhuru Kenyatta atupe bajeti ya ziada ya angalau Sh5 bilioni ili tuweze kumudu gharama ya kujianda kukabiliana na janga hili kama vile kuweka vitanda zaidi maalum vya kuwahudumia wagonjwa wa Covid-19.”
Naye Bw Wamalwa amezitaka taasisi zote za serikali kuungana katika vita dhidi ya janga hili.
“Nawaomba madiwani wetu kusitisha vita vyao na magavana wakati huu ambapo janga la corona linaathiri maisha ya watu wetu. Waelekeze juhudi zote katika vita dhidi ya adui huyo. Huu sio wakati wa kuondoa huyu au yule mamlakani,” akaeleza.
Bw Wamalwa amesema viwango vya maambukizi ya virusi vya corona vinatarajiwa kuwa juu zaidi kuanzia mwezi ujao wa Julai hadi Septemba, hivyo kaunti zinafaa kujiandaa kukabiliana na ongezeko la idadi ya wagonjwa wanaohitaji kulazwa.
“Vita vinavyoendelea sasa havitatusaidia kukabiliana na changamoto hii ya kiasi bali vitaathiri hatua ambazo tumepiga kufikia sasa,” akasema.
Baada ya jaribio la madiwani wa Kirinyaga kumwondoa mamlakani Gavana Anne Waiguru kutibuka Ijumaa wiki jana, wiki hii madiwani wa Kitui wanapanga kupitisha hoja ya kutokuwa na imani na Gavana Charity Ngilu.
Magavana wengine wanaokabiliwa na tishio la hoja kama hizo ni Patrick Khaemba (Trans-Nzoia), Salim Mvurya (Kwale) na Wycliffe Wangamati (Bungoma).