Michezo

Real Madrid yafungua mwanya wa alama mbili kileleni mwa La Liga

June 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

REAL Madrid walisajili ushindi wa 1-0 dhidi ya Espanyol uwanjani RCDE mnamo Jumapili usiku na kufungua pengo la alama mbili kati yao na mabingwa watetezi Barcelona kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Bao la hilo la pekee lilifumwa wavuni na kiungo matata mzawa wa Brazil, Carlos Henrique Casemiro aliyeshirikiana vilivyo na fowadi Karim Benzema na kumwacha hoi beki Bernardo Espinosa wa Espanyol kunako dakika ya 45.

Casemiro alikuwa awali amepoteza nafasi mbili za wazi baada ya kupaisha mpira licha ya kusalia uso kwa macho na kipa Diego Lopez.

Fursa tano ambazo Espanyol walizipata langoni pa Real kupitia kwa mshambuliaji Wu Lei, zilizimwa kirahisi na kipa Thibaut Courtois anayetarajiwa kuhudumu uwanjani Santiago Bernabeu hadi mwaka wa 2024 baada ya kutia saini mkataba wa miaka sita alipoondoka Chelsea mnamo Agosti 2018.

Mechi dhidi ya Real ilikuwa ya kwanza kwa mkurugenzi wa spoti kambini mwa Espanyol, Francisco Rufete, kusimamia baada ya kuaminiwa mikoba ambayo mkufunzi Abelardo Fernandez alipokonywa mnamo Jumamosi iliyopita kutokana na matokeo duni. Fernandez ndiye kocha wa tatu kufutwa kazi na Espanyol hadi kufikia sasa msimu huu.

Chini ya kocha Zinedine Zidane, Real kwa sasa wanahitaji kusajili ushindi mara sita au hata kujizolea alama 16 pekee kutokana na michuano sita iliyosalia katika kampeni za La Liga msimu huu ili kutawazwa mabingwa wa soka ya Uhispania kwa mara ya kwanza tangu 2012.

Hesabu zao pia za kujinyakulia ubingwa wa muhula huu zitategemezwa kwa matokeo ya mechi itakayowakutanisha Barcelona na Atletico Madrid uwanjani Nou Camp mnamo Alhamisi ya Julai 2, 2020.

Ushindi kwa Atletico katika gozi hilo itakuwa afueni na hisani kubwa kwa Real wanaowinda taji lao la 34 la La Liga.

Bao la dakika za mwisho kutoka kwa mvamizi matata mzawa wa Uhispania, Iago Aspas, 32, liliwawezesha Celta Vigo kuwabana Barcelona kwa 2-2 na kuzamisha kabisa matumaini ya miamba hao wa La Liga kuhifadhi ubingwa wa msimu huu.

Kufikia sasa, Espanyol wanavuta mkia wa jedwali la La Liga kwa alama 24 na wapo katika hatari ya kushushwa ngazi kwa pamoja na Leganes na Mallorca wanaojivunia alama 25 na 26 mtawalia.

Real wanaselelea kileleni kwa alama 71, mbili zaidi kuliko nambari mbili Barcelona. Pengo la pointi nne linatamalaki kati ya nambari tatu Atletico na Sevilla wanaofunga orodha ya nne-bora kwa alama 54.