Michezo

DIMBA: Kwa chenga tu, mwachie Pulisic

June 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

CHIPUKIZI Christian Pulisic kutoka Amerika anafahamika kwa kasi ya kutisha na chenga zake.

Kinda huyu ambaye pia huitikia majina ya utani ‘Manni’ na ‘Captain America’, ni mali ya klabu ya Chelsea inayoshiriki Ligi Kuu Uingereza(EPL).

Ni winga wa pembeni kushoto aliye pia na uraia wa Croatia. Pulisic alizaliwa Septemba 18, 1998 mjini Hershey katika jimbo la Pennsylvania nchini Amerika.

Ni kitindamimba katika familia inayoenzi soka na kufuata nyayo za wazazi wake Mark Pulisic (babake) na Kelley Pulisic (mamake), ambao walisakata soka katika Chuo Kikuu cha George Mason katika jimbo la Virginia.

Babake ni naibu kocha wa timu ya Pittsburgh Riverhounds SC inayoshiriki Ligi ya Daraja ya Pili nchini Amerika. Naye dadake, Dee Dee, pia alicheza soka akiwa mdogo. Hivyo, winga huyu amelelewa akipenda kabumbu.

Pulisic alianza kuona mwanga katika soka yake mnamo 2005 mamake alipopata kazi ya kufundisha nchini Uingereza. Familia ikahamia mtaa wa Tackley kaskazini mwa mji wa Oxford.

Babake hakupoteza muda kumuingiza katika akademia ya soka katika mji jirani wa Brackley. Hii ilimpata Pulisic nafasi nzuri ya kukuza mchezo wake kwa mwaka mmoja akishiriki katika mashindano ama kucheza katika bustani na viwanja mbalimbali.

Ukuaji wake ulifurahisha sana wazazi wakammsajili katika timu ya Michigan Rush waliporejea nchini Amerika. Akachezea timu hiyo ya jimbo la Michigan kwa miezi kadha kabla kurejea na familia yake mtaani Hershey.

Wazazi wakaamua kumuandikisha katika akademia ya ukuzaji talanta ya Pennsylvania Classics, Amerika. Kwa miaka saba kiungo huyu alipata fursa ya kusakata soka dhidi ya makinda wenzake na hata baadhi waliomzidi umri.

Pulisic kisha alipiga hatua kubwa katika soka yake alipojiunga na Borussia Dortmund mnamo Februari 2015 kutoka Pennsylvania Classics.

Alipata fursa ya kuchezea timu ya watu wazima ya klabu hiyo ya Ujerumani mnamo Januari 30, 2016, alipoingizwa katika kipindi cha pili kama mchezaji wa akiba. Dortmund ililemea Ingolstadt 2-0.

Miezi miwili baadaye, aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Amerika, Jurgen Klinsmann, alimjumuisha katika kikosi kilichovaana na Guatemala kwa majukumu ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2018. Alijaza nafasi ya Graham Zusi katika dakika ya 81 na kuwa mchezaji mwenye umri mdogo kuwahi kuchezea Amerika katika mechi ya kuwania tiketi ya Kombe la Dunia. Amerika walilima Guatemala 4-0.

Kwa kuchezea Amerika mechi ya kimataifa, Pulisic alipoteza kibali cha kusakatia pia Croatia, kwani huwezi wakilisha mataifa mawili.

Mchezaji huyo alivunja rekodi kadha nchini Ujerumani ikiwemo ile ya kuwa mwanasoka mwenye umri mdogo wa Dortmund kuwahi kushiriki Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Alipata umaarufu mkubwa akiwa Dortmund alipoisaidia kunyakua Kombe la Ujerumani (DFB Pokal) kabla ya Chelsea kumnyaka Januari 3 mwaka jana kwa kitita cha Sh7.6 bilioni. Alirejeshwa Dortmund kwa mkopo hadi Juni 30, 2019.

Aliporejea uwanjani Stamford Bridge msimu huu wa 2019-2020, haikumchukua muda kabla kuweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi wa Chelsea kupata mabao matatu katika mechi moja, aliposaidia Blues kuzamisha Burnley 4-2 ligini mnamo Oktoba 26, 2019.

Pulisic amechezea Chelsea mechi 18 za ligi ikiwemo kukaribishwa kwa kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Manchester United mwezi Agosti, na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya waliokuwa mabingwa watetezi, Manchester City, Alhamisi iliyopita.

Kijana huyu anakula mshahara wa Sh19.1 milioni kila wiki kambini mwa Chelsea. Ana mali ya thamani ya Sh1.6 bilioni. Mapato yake pia yanatokana na kutangaza bidhaa za kampuni tofauti zikiwemo chokoleti, kakao, vinywaji na vifaa vya michezo.