Makala

TAHARIRI: Uchochezi usipewe nafasi humu nchini

June 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

TAHARUKI ya kisiasa imeanza kupanda mapema kabla tufikie kipindi rasmi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Ijapokuwa kwa muda mrefu tumeshuhudia viongozi wa kisiasa wakizozana hadharani, inatia hofu jinsi sasa malumbano haya yanashika kasi.

Tumesalia na takriban miaka miwili pekee kabla uchaguzi ufanywe na kila mwanasiasa ameanza kujinadi kwa kila njia ikiwemo kutumia uchochezi wa jamii.

Matukio ambayo yanashuhudiwa katika kaunti mbalimbali hivi sasa ni ya kushtua na inahitajika yazimwe mara moja.

Visa vya uchochezi wa kijamii vinazidi kuongezeka katika pembe tofauti za nchi.

Hivi ni visa ambavyo kwa miaka mingi vimekuwa vikichochewa na wanasiasa wanaojitafutia makuu ya kibinafsi bila kujali athari zinazotokea kwa umma.

Asasi zilizotwikwa jukumu la kukabiliana na wachochezi ni sharti zikaze kamba. Inaaminika kuna baadhi ya wanasiasa ambao walidhani watakwepa mkono wa sheria wakichochea umma, kisha waende kujitetea mahakamani kwamba walikuwa wanatimiza haki yao ya uhuru wa kujieleza.

Ni kweli kuwa uhuru wa wananchi wa Kenya kujieleza ni haki iliyolindwa kikatiba, lakini ifahamike haki ya mtu mmoja haipaswi kufanya wengine wakose haki zao.

Uchochezi ni jambo hatari ambalo linaweza kusababisha ghasia na kupokonya wananchi haki zao, ikiwemo haki ya maisha kwani wengi huuliwa baada ya jamii kuchochewa dhidi ya nyingine na wanasiasa.

Haki nyingine ambazo huwa hatarini kunapotokea uchochezi ni kama vile watu kukosa makao bora kwani wengi hufurushwa katika makazi yao na huishia kuishi katika makambi ya wakimbizi.

Kando na wanasiasa, inahitajika jamii nzima kwa jumla kutambua hatari wanayojiletea kila mara wanapokubali kuchochewa na wanasiasa kushambulia wenzao.

Wananchi wanastahili kusimama wima kuwalazimisha viongozi wa kisiasa kutekeleza majukumu yao ambayo yataboresha hali ya maisha badala ya kutegemea hela kidogo wanazopewa kwenda kudhuru majirani wao.

Licha ya watu kushuhudia madhara mengi yanayotendwa kwa raia na taifa kwa jumla ghasia zinapotokea popote pale, bado wengine hushawishika kwa pesa nane kujihusisha kwa vitendo hivyo.

Inasikitisha jinsi wengi wanaochochewa huwa ni vijana ambao ndio tegemeo kuu la uongozi bora na uimarishaji uchumi wa nchi hii.