• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 2:55 PM
TAHARIRI: Kenya ifuatilie kwa makini virusi vipya

TAHARIRI: Kenya ifuatilie kwa makini virusi vipya

Na MHARIRI

WAKATI umewadia kwa Serikali kuwekeza rasilimali zaidi katika sekta ya afya ambayo kwa miaka mingi ilipuuzwa na marais waliotangulia.

Umuhimu wa sekta hiyo bila shaka umedhihirika wazi wakati huu ambapo kumekuwa na mkurupuko wa virusi hatari vya corona ambavyo vimetetemesha ulimwengu kwa namna vinavyosambaa kwa kasi.

Kwenye ruwaza ya serikali kuhusu maendeleo, serikali imekuwa akiahidi itahakikisha watu na jamii zote wanapokea huduma za afya bila kujali uwezo wao wa kifedha.

Huduma hizo zinajumuisha huduma muhimu za afya kama vile kutoa kinga na kutibu pamoja na kutunza wale waliolemewa na maradhi.

Huu ndio wakati mwafaka wa kununua vifaa vya kisasa vya matibabu na kuwapa wauguzi wetu fursa ya kujinoa zaidi, hasa kutokana na habari kwamba, aina mpya ya virusi ambavyo vinasambazwa kupitia kwa nguruwe vimepatikana nchini China.

Watafiti wanasema virusi hivyo, G4 EA H1N1 vinashambulia na kusambaa kwenye mfumo mzima wa binadamu wa kupumua. Wanasayansi walipata ushahidi wa virusi hivyo katika watu walioambukizwa kwenye vichinjio vya nguruwe China.

La kuhofisha ni kwamba, chanjo zote za homa zilizopo haziwezi kumkinga mwathiriwa dhidi ya maambukizi. Kimsingi, kile wanasayansi hao wanasema ni kwamba, aina hii ya homa ina uwezo wa kugeuka kuwa janga kama lile la corona ambalo limeangamiza zaidi ya watu 500,000 kote duniani na kuambukiza zaidi ya milioni sita.

Kuna mengi ambayo janga la sasa limefunza viongozi, hasa wale wa mataifa ya Afrika.

Kujiandaa mapema kwa hali zote ni muhimu katika kuhimili athari za maambukizi ya virusi vinavyosambaa kwa kasi.

Mojawapo ya sababu ambazo zimewezesha Wakenya na mataifa mengi ya Afrika kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo ni hatua za haraka zilizochukuliwa na serikali za mataifa hayo.

Mataifa ya Ulaya na Amerika ambayo yalipuuza au kuamini kupita kiasi uwezo wao wa kukabiliana na virusi hivyo yamepoteza maelfu ya raia wao.

Vijiji vizima viliangamia katika mataifa kama Italia. Amerika ingali bado inatapatapa huku awamu ya pili ya virusi hivyo ikiathiri majimbo kadha ya taifa hilo kubwa.

Wizara ya Afya imefanya kazi nzuri katika kuhamasisha Wakenya kuhusu namna ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi hivyo.

Huu ndio wakati tena wa kuwa macho ili virusi hivyo vipya visiwahi kutua nchini tena.

You can share this post!

BAJETI: Waiguru akatwa miguu na MCAs

Ashauri KWS tumbili wapangishwe uzazi

adminleo