Ashauri KWS tumbili wapangishwe uzazi
LUCY MKANYIKA na MISHI GONGO
MBUNGE wa Wundanyi, Bw Danson Mwashako ameitaka Idara ya Huduma za Wanyama Pori (KWS) kudhibiti idadi ya tumbili ambao wanasababisha hasara kwa wakulima wa eneo hilo.
Bw Mwashako alisema KWS inafaa kutumia njia ya upangaji uzazi kwa wanyama hao waharibifu ili kuzuia ongezeko la idadi yao.
Alisema wanyama hao ambao wamekuwa wakizaana kwa kasi wamevamia mashamba na kusababishia wakulima hasara na hivyo kutishia uzalishaji chakula kwa kiwango cha kutosheleza mahitaji ya wakazi katika eneo hilo.
“Wenyeji wengi wa eneo hili hutegemea kilimo ili kujikimu kimaisha. Tumbili hawa wamekuwa kero kwa wakulima ambao sasa wamekufa moyo na hivyo kuwacha shughuli za ukulima,” akasema.
Bw Mwashako alidai kuwa juhudi za kutafuta usaidizi kutoka kwa idara ya KWS ziliambulia patupu kwani hadi sasa hakuna suluhu yeyote waliotoa.
Wanyama hao ambao hujificha katika milima ya Taita wamekuwa kero kwa wakulima ambao juhudi zao za kuwatoa hazijazaa matunda.
Licha ya kutumia mbinu mbalimbali zikiwemo kuweka vinyago shambani, wanyama hao wanaendelea kuvamia mimea yao na kusababisha hasara isiyokadirika.
“Sasa inatulazimu tufanye zamu ya kulinda mashamba. Tumbili hawa hupenda kula maharagwe, mahindi, avocado na wakati mwingine wao hula hata miwa,” akasema mkulima mmoja Bw Johnstone Makumbi.
Licha ya hasara wanayopata kutokana na wanyamapori wanaotoroka mbuga ya Tsavo, serikali imekawia kutoa fidia kwa waathiriwa wa mikasa hiyo.
Hata hivyo, hivi majuzi serikali ilitangaza kuwa imetoa fidia ya takriban Sh78 milioni kwa baadhi ya waathiriwa na kuahidi kutenga fedha zingine ili kumalizia kulipa madeni hayo.
Msimamizi wa eneo la Tsavo Bw Robert Njue alisema kuwa wametuma maafisa wa shirika la KWS ili kusaidia wenyeji kutatua kero hiyo.
“Tumeongea na viongozi wa eneo hilo na tujakubaliana njia ya kusaidiana nao,” akasema.
Kwingineko, afisa wa kulinda misitu katika Kaunti ya Kwale amewaonya wanaoendeleza biashara haramu ya makaa na wanaokata misitu ovyo.
Bw George Wara alisema biashara hiyo inachangia pakubwa katika kuleta uhasama kati ya binadamu na wanyamapori mbali na kuharibu mazingira.
Alitaja maeneo ya Lunga Lunga, Samburu na Puma kuwa maeneo sugu ya watu wanaoendeleza biashara hiyo.
“Wakazi wanaoishi katika sehemu kavu za kaunti hii ndiyo wanaendeleza biashara hii. Tutahakikisha kuwa anayekamatwa anachukuliwa hatua kali ili kudhibiti biashara hii haramu,” akasema.