• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Maafisa wafuatilia visa vya dhuluma za kingono Kwale

Maafisa wafuatilia visa vya dhuluma za kingono Kwale

Na MISHI GONGO

MAAFISA wa serikali wameanza kufuatilia visa vya dhuluma za kingono ambavyo haviripotiwi katika eneo la Mivumoni, Msambweni katika Kaunti ya Kwale.

Chifu wa eneo hilo Bw Thomas Ngangi alisema hatua hiyo itawasaidia watoto waliyodhulumiwa kimapenzi kupata haki.

Alieleza kuwa eneo hilo linakumbwa na visa vingi vya watoto kudhulumiwa kimapenzi bila kuripotiwa katika idara husika.

“Visa vingi vya dhuluma kwa watoto hutatuliwa nyumbani hivyo kuwanyima watoto haki,” akasema.

Ngangi alieleza kuwa kuna ongezeko la visa vya ulawiti na unajisi katika eneo hilo ambavyo havijaripotiwa ili wahalifu waweze kuchukuliwa hatua.

Alisema hali hiyo imechangia kuongezeka kwa visa hivyo kutokana na wahalifu hao kukwepa mkono wa sheria.

Chifu huyo alisema miongoni mwa visa wanavyopokea ni vile vya watoto kunajisiwa na jamaa zao wa karibu.

“Kuna baadhi ya wazazi ambao kwa kuhofia aibu huamua kutatua dhuluma hizi kinyumbani; hasa kama aliyetekeleza kitendo ni jamaa wa karibu,” akasema.

Hata hivyo, chifu huyo aliwaonya wazazi dhidi ya kuwaweka pamoja watoto wa jinsia tofauti akidai kwamba huenda ikawa chanzo cha kuzuka kwa visa hivyo katika jamii.

Alieleza kuwa mtoto wa kiume hajasazwa katika kukumbana na dhuluma sawia na mtoto wa kike.

You can share this post!

Ashauri KWS tumbili wapangishwe uzazi

Bei ya unga kushuka

adminleo