ZUIO: Nyumba za wapangaji waliofungiwa nje ya Nairobi zavunjwa makufuli mmiliki akiweka yake
Na SAMMY WAWERU
VISA vya malandilodi kuvunja nyumba za wapangaji waliofungiwa nje ya Nairobi kufuatia amri ya kutotoka nje na kuingia kaunti hiyo vimeanza kushuhudiwa.
Siku kadhaa baada ya Kenya kuripoti kisa cha kwanza cha maambukizi ya Covid-19, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuanza kutekelezwa kwa amri hiyo kama njia mojawapo ya kuzuia msambao zaidi.
Ilianza kutekelezwa Machi 27, 2020, ambapo kiongozi wa nchi aliagiza zuio hilo la usafiri kwa siku 21 na mnamo Aprili 25, 2020, akatangaza kurefushwa kwa siku 21 zaidi ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.
Mei 6, 2020, Rais Kenyatta alirefusha tena zuio hilo kwa siku 30 zaidi.
Aidha, baadhi ya wakazi wa Nairobi na waliokuwa wametembea mashambani wakati kukitangazwa amri hiyo kwa mara ya kwanza, walifungiwa huko na imebainika malandilodi kadhaa wameanza kuvunja nyumba za walioshindwa kulipa kodi.
Katika mtaa wa Zimmerman, Nairobi Jumanne jioni landilodi wa ploti moja ya kupangisha aliagiza nyumba za waliofungiwa nje ya Nairobi makufuli yavunjwe mara moja, akilalamikia kukadiria hasara kwa muda wa miezi mitatu mfululizo.
Mmiliki alinukuliwa akidai “kodi imekusanyika na inayojumuisha miezi kadhaa kabla ya janga la corona na ninataka kujua nitakavyolipwa”.
Oparesheni hiyo iliyoongozwa na chifu wa eneo la Zimmerman aliyeandamana na afisa mmoja wa polisi, ilipelekea nyumba kadhaa kuvunjwa kufuli za wapangaji kuondolea mmiliki akitia zake.
“Tumekuwa tukiwapigia simu hawapokei, ilhali kodi inaendelea kukusanyika,” James Kithome, keateka wa ploti akaeleza wakati wa shughuli hiyo.
Kupitia barua iliyotazamwa na Taifa Leo, wapangaji wanaodaiwa wametakiwa wafike kwa chifu hii leo, Jumatano, Julai 1, 2020, la sivyo wachukuliwe hatua.
Ikiwa walifungiwa nje ya jiji haieleweki watafika hapo kwa jinsi gani.
Hata hivyo, imebainika baadhi ya kodi wanayodaiwa imechakachuliwa. “Wengine wetu hasa tulioingia majuzi hatuna deni, na tunadaiwa kodi za waliotutangulia,” wapangaji kadhaa wakalalamika.
Isitoshe, kuna barua za nyumba zisizo na wapangaji zilitumwa. Juhudi za kufikia mmiliki wa ploti hiyo kujibu malalamishi ya wapangaji hazikufua dafu, tulipomfikia kwa njia ya simu alituelekeza kwa keateka wake.
Imefichuka wengi wa wapangaji waliopoteza ajira na biashara zao kufilisika Nairobi, kufuatia athari za corona wanapitia madhila kama hayo.
“Nimefungiwa nyumba mara kadhaa kati ya mwezi Aprili na Juni. Mshahara wangu ulisimamishwa mwishoni mwa Machi 2020, nina familia, ni kodi ya nyumba nitalipa au ni watoto nitalisha?” akahoji mkazi.