Michezo

Messi afikisha mabao 700 kitaaluma Barcelona wakiambulia sare ya 2-2 dhidi ya Atletico Madrid

July 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

LIONEL Messi alifunga bao lake la 700 katika taaluma ya usakataji wa soka mnamo Juni 30, 2020 na kusaidia Barcelona kusajili sare ya 2-2 dhidi ya Atletico Madrid uwanjani Camp Nou.

Messi aliweka rekodi hiyo katika ngazi ya timu ya taifa na klabu kupitia penalti ya dakika 50 iliyomwacha hoi kipa Jan Oblak anayehemewa sana na Manchester United.

Bao hilo la Messi liliwaweka Barcelona uongozini kwa magoli 2-1 kabla ya Atletico kusawazishiwa na Saul Niguez katika dakika ya 62. Awali, mshambuliaji Diego Costa alikuwa amejifunga katika dakika ya 11 kabla ya Niguez kusawazisha mambo dakika nane baadaye.

Matokeo hayo yanasaza Barcelona katika nafasi ya pili kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kwa alama 70, moja nyuma ya Real ambao watakuwa wenyeji wa Getafe mnamo Alhamisi ya Julai 2, 2020.

Penalti iliyofungwa na Messi ilikuwa yake ya 630 na mechi hiyo dhidi ya Atletico ilikuwa yake ya 724 ndani ya jezi za Barcelona. Messi ndiye alichangia pia bao la kwanza ambalo Barcelona lililofumwa wavuni na Costa aliyejifunga.

Fadhaa zaidi kwa Costa katika gozi hilo ni kushuhudia penalti yake ikipanguliwa na kipa Marc-Andre ter Stegen. Penalti hiyo iliyofungwa baadaye na Niguez katika jaribio la pili, ilikuwa zao la kuchezewa vibaya kwa mshambuliaji Yannick Carrasco. Mkwaju wa Costa ulifutiliwa mbali na refa kwa madai kwamba Ter Stegen alikuwa ametoka kwenye mstari wa goli.

Messi alifunga bao lake la 700 kitaaluma miezi 14 pekee baada ya kupachika wavuni goli lake la 600 akivalia jezi za Barcelona.

Anaingia kwa sasa katika orodha ya wanasoka saba kuwahi kupachika wavuni jumla ya mabao 700 katika taaluma zao za usogora.

Josef Bican ambaye ni mzawa wa Jamhuri ya Czech na raia wa Austria anaongoza orodha ya wafungaji bora wa muda wote katika historia ya soka kwa mabao 805 akifuatwa na nguli wa Brazil, Romario de Souza Faria aliyefunga mabao 772 katika enzi yake. Edson Arantes do Nascimento ‘Pele’ ambaye pia ni mzawa wa Brazil anashikilia nafasi ya tatu kwa mabao 767.

Nguli wa Hungary, Ferenc Puskas alifunga mabao 746 huku mvamizi wa zamani wa Ujerumani, Gerd Muller akifunga orodha ya tano-bora kwa mabao 735.

Mshindani mkuu wa Messi, Cristiano Ronaldo anashikilia nafasi ya sita kwa mabao 726.

Messi anajivunia kufunga zaidi ya mabao 40 katika ngazi ya klabu na timu ya taifa kila mwaka katika kipindi cha miaka 11 iliyopita na zaidi ya mabao 50 kila mwaka katika kipindi cha miaka tisa kati ya 10 iliyopita. Kufikia sasa mwaka huu wa 2020, anajivunia jumla ya mabao 11 licha ya kalenda ya soka kuvurugwa na janga la corona kwa kipindi cha miezi mitatu.

Katika ya vikosi 40 ambavyo Messi amekabiliana navyo katika historia ya soka ya Uhispania kufikia sasa, hajafunga dhidi ya vitatu pekee. Klabu hizo ni Xerez, Real Murcia na Cadiz.

Kati ya mabao yote 700 ambayo Messi amefunga katika taaluma yake, 582 yametokea kwenye guu lake la kushoto huku akipachika wavuni 92 mengine kwa kutumia mguu wa kulia na 24 kwa kutumia kichwa.

Mabao 52 yametokana na mipira ya ikabu au frikiki za moja kwa moja huku 90 yakiwa ya mikwaju ya penalti.