Makala

GWIJI WA WIKI: Maria Mvati

July 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 4

Na CHRIS ADUNGO

INAWEZEKANA hujui kipaji chako au hujajibidiisha kabisa kukitambua.

Pengine umekidharau kwa kudhania kwamba talanta za wengine ni bora zaidi kuliko chembechembe za usanii ulizo nazo.

Jisake upya, jitambue na ujitume kwa kuwa mafanikio ni zao la imani, bidii, nidhamu na stahamala!

Kufaulu katika jambo lolote kunahitaji mtu kuwa na maono na kutenda mema bila ya kudhamiria malipo. Jikubali jinsi ulivyo na uache kujilinganisha na watu wengine.

Lenga kuwa bora katika chochote unachoteua kukishughulikia na umweke Mungu mbele siku zote kwa kuwa ndiye mwelekezi wa kila hatua tunayoipiga maishani na kitaaluma.

Huu ndio ushauri wa Bi Maria Navulia Mvati; mwandishi maarufu na mshairi shupavu aliyewahi kufundisha Kiswahili katika Shule ya Upili ya State House Girls, Nairobi.

MAISHA YA AWALI

Maria alizaliwa na kulelewa katika eneo la Pare-Same, Mkoa wa Kilimanjaro, Tanzania. Yeye ni mzaliwa wa sita katika familia ya watoto 11 wa marehemu Bw Ombeni Fundi Sekiete Mgonja na marehemu Bi Navoneiwa Makoko.

Alianza safari yake ya elimu mnamo 1965 katika Shule ya Msingi ya Misheni ya Vumari iliyoko katika Dayosisi ya Kanisa Katoliki ya Pare-Same na akaufanya mtihani wa mwisho wa darasa la saba katika mwaka wa 1971.

Alama nzuri alizozipata zilimpa nafasi ya kujiunga na Shule ya Upili ya Machame Girls katika eneo la Kilimanjaro, Wilaya ya Moshi, Tanzania mnamo 1972.

Alihitimu Hati ya Masomo ya Kidato cha Nne mwishoni mwa 1975 na kujiunga na Shule ya Upili ya Jangwani, Dar es Salaam, Tanzania kwa minajili ya kusomea kiwango cha ‘A-Levels’ kati ya 1976 na 1977.

Alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa kwanza kushirikishwa katika mfumo mpya wa masomo ya sanaa (Historia, Jiografia na Kiswahili) katika shule hiyo iliyokuwa maarufu sana kwa mfumo wa masomo ya sayansi (Fizikia, Kemia na Hisabati).

Mnamo Julai 1978, Maria alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mafunzo na mazoezi ya kijeshi ambayo ni ya lazima kwa wanafunzi wote wanaofuzu kujiunga na vyuo vikuu kwa ufadhili wa Serikali nchini Tanzania.

JKT lina jukumu la kuwalea vijana wa Tanzania kinidhamu na kuwafundisha ujuzi wa kuchangia ulinzi wa taifa na maendeleo ya kiuchumi kwa uzalendo, umoja na ukakamavu zaidi.

Maria alihudumu katika kambi ya taifa ya Makutupora, Dodoma kwa kipindi cha mwaka mmoja kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusomea taaluma ya ualimu kati ya 1979 na 1983. Akiwa Makutupora, aliaminiwa kuwa msimamizi wa makurutu na akawa kiongozi wao katika mafunzo mbalimbali ya kinadharia na shughuli za ukuzaji wa zabibu.

UALIMU

Baada ya kuhitimu ualimu mnamo 1983, Maria alianza kufundisha katika Shule ya Upili ya Nganza, Mkoa wa Mwanza, Tanzania. Alihudumu huko kwa kipindi cha miezi sita kabla ya kuhamia Shule ya Upili ya Ruvu, eneo la Muhimbili, Dar es Salaam alikofundisha hadi Julai 1984.

Mwaka huo ndipo alipoolewa na mumewe mpendwa, Bw Martin Matayo Mvati ambaye amekuwa nguzo muhimu katika safari ya makuzi yake kitaaluma.

Mnamo Oktoba 1984, Maria alihamia Kenya na kuanza kufundisha Kiswahili katika Shule ya Upili ya State House Girls, Nairobi akiwa mwalimu wa msimu.

Ilikuwa hadi mwaka wa 1990 alipoajiriwa rasmi na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) baada ya kupata uraia wa Kenya.

Hadi alipostaafu mnamo Julai 2016 Maria alikuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili, Mtahini wa Kitaifa wa Fasihi ya Kiswahili na Mkuu wa Idara ya Ushauri Nasaha katika Shule ya Upili ya State House Girls.

UANDISHI

Maria anaamini kwamba uandishi ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani yake tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Mengi ya mashairi aliyokuwa akitunga na kughani yalimvunia tuzo za haiba kubwa na za kutamanisha mno katika tamasha za kitaifa za muziki na drama.

Kati ya waliompulizia hamu ya kuandika zaidi ni Profesa Abdilatif Abdalla aliyewahi kualikwa na shule yao ya Jangwani Girls kutoa hotuba ya kuwatia motisha wanafunzi wa kidato cha sita kuhusu umuhimu wa kuchangamkia Kiswahili na manufaa yake katika siku za baadaye.

Mnamo 1995 Maria alishirikiana na marehemu Bi Salome Maneno na Bi Maliachi kuandika kitabu ‘Nuru ya Ushairi’ kilichochapishwa na Kenya Literature Bureau (KLB).

Mwaka mmoja baadaye, alishirikiana tena na Bi Maneno kuandika kitabu ‘Mazoezi na Marudio ya Kiswahili’ kilichofyatuliwa na KLB.

‘Peak Revision Course’ ni kitabu ambacho Maria aliandika kwa kushirikiana na Bw Hassan Makombo na Bw Andrew Watuha. Kilitolewa na East African Educational Publishers (EAEP) mnamo 2006, mwaka mmoja baada ya Franciscan Kolbe Press Limuru kuchapisha kitabu ‘Mwangaza wa Fasihi Simulizi’ alichokiandika kwa pamoja na Bw Kiarie Kiongera, Bw James Kanuri na marehemu Bi Mary Kubo.

Vitabu vingine ambavyo Maria ametunga kwa kushirikiana na waandishi wenzake katika Shirika la Huduma za Kielimu kwa Taifa (NES) hususan Bw Kanuri, Bw Kiongera, Bi Salyne Nyongesa, Bi Rachael Maina na Bw Simon Kanyingi ni msururu wa ‘Miale ya Isimujamii’, ‘Miale ya Ushairi’, ‘Miale ya Sarufi’ na ‘Miale ya Insha’.

Mbali na kuandika kitabu ‘Kiswahili Taaluma kwa Darasa la Kwanza’ kilichochapishwa na Pamita Booksellers & Publishers mnamo 2013, Maria amewahi pia kutunga ‘Miongozo ya Walimu’ kwa vitabu ‘Chemchemi za Kiswahili’ (K. W. Wamitila) na miongozo ya vitabu mbalimbali vya fasihi vilivyowahi na vinavyotahiniwa kwa sasa katika KCSE Kiswahili.

Anaandaa sasa miswada ya hadithi fupi na ushairi wa Kiswahili kwa matarajio kwamba kazi hizo zitachapishwa hivi karibuni.

JIVUNIO

Uzoefu wa kushiriki na kuwasilisha makala katika makongamano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa umemwezesha Maria kutangamana na watalaamu wengi wa lugha.

Anajivunia kuandaa na kuhudhuria warsha nyingi katika sehemu mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kukipigia chapuo Kiswahili, kuwaelekeza na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya KCSE Kiswahili.

Katika kipindi cha zaidi ya miongo mitatu ya ualimu, Maria amefundisha idadi kubwa ya wataalamu na wasomi ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili.

Kwa pamoja na mumewe Bw Mvati ambaye ni mzaliwa wa Kaunti ya Taita-Taveta, wamejaliwa watoto watatu: Navuri, Joel na Kenneth.