Amina aunda kamati ya kuishauri wizara yake jinsi michezo itakavyorejelewa nchini
Na CHRIS ADUNGO
WAZIRI wa Michezo, Amina Mohamed ameunda kamati ya watu 18 kutathmini mapendekezo ya wadau mbalimbali na kushauri Serikali kuhusu uwezekano na taratibu za kurejelewa kwa shughuli za michezo humu nchini.
Tangu kisa cha kwanza cha corona kiripotiwe humu nchini mnamo Machi 13, 2020, Serikali ilipiga marufuku mikusanyiko yote ya umma na kusitisha shughuli zote za michezo.
Hatua hiyo ilikuwa pigo kubwa kwa wanamichezo waliokuwa wakijiandaa kwa mapambano mbalimbali katika ngazi za watu binafsi au timu. Hii ni baada ya Serikali kupiga marufu ziara zote za nje ya nchi na kuweka masharti makali, ikiwemo kafyu, ili kudhibiti msambao zaidi wa virusi vya homa kali ya corona.
Kamati iliyoundwa na Amina itaongozwa na Katibu Mratibu wa Wizara ya Michezo, Hassan Noor Hassan na itajumuisha pia washikadau mbalimbali kutoka idara mbalimbali za serikali, mashirikisho ya michezo tofauti na vyombo vya habari.
Kamati inatarajiwa kushauriana na mashirikisho ya michezo mbalimbali ya humu nchini ili kupata mapendekezo yao kuhusu jinsi ya kufunguliwa rasmi kwa ulingo wa spoti na hatimaye kutoa utaratibu na mwelekeo mwafaka utakaofanikisha mchakato huo.
Kamati inatarajiwa pia kupendekeza hatua zitakazofuatwa baada ya kutathmini hali ilivyo katika baadhi ya mataifa ambayo yamerejelea shughuli za michezo bila ya mahudhurio ya mashabiki uwanjani.
Mnamo Aprili 2020, Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) ilitoa mwongozo wa afya ambao mataifa wanachama yalistahili kutekeleza kabla ya kurejelea mchezo wa kabumbu. Maoni yote kuhusu jinsi kandanda ya humu nchini itakavyorejelewa sasa yatashughulikiwa na daktari wa kipindi kirefu kambini mwa Harambee Stars na Tusker FC, Wycliffe Makanga.
Masuala yanayohusiana na riadha yatashughulikiwa na Barnaba Korir ambaye ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) Tawi la Nairobi na kinara wa masuala ya maendeleo wanariadha chipukizi katika AK.
Baada ya Michezo ya Olimpiki kuahirishwa hadi 2020 na maandalizi kusitishwa, Katibu Mkuu wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki (Nock), Francis Mutuku atashauri Wizara ya Michezo kuhusiana na athari ambazo zimeletwa na janga la corona kwenye ulingo wa riadha huku mhariri veterani wa masuala ya michezo, Elias Makori wa Nation Media Group (NMG) akiwakilisha matamanio ya wanahabari.
Wengine katika kamati hiyo ya Amina ni Msajili wa Michezo Rose Wasike, Mkurugenzi wa Sports Kenya Pis Meto na Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirika la kukabiliana na matumizi ya pufya nchini (ADAK), Japhter Rugut.
Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Kenya Academy of Sports Doreen Odhiambo, Rais wa Kamati ya Olimpiki za Walemavu Agnes Oluoch na Kamishna wa Michezo Gerald Gitonga wanakamilisha orodha ya kamati hiyo inayotarajiwa kuwasilisha ripoti yao kufikia Julai 10, 2020.