• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
Korti yaamua polisi alibaka mwanamke akipiga ripoti katika kituo

Korti yaamua polisi alibaka mwanamke akipiga ripoti katika kituo

Na KALUME KAZUNGU

KONSTEBO wa polisi amepatikana na hatia ya kumbaka mwanamke aliyekuwa ameenda kupiga ripoti katika kituo cha polisi cha Lamu mwaka 2019.

Rodgers Ouma, 32, anayehuduma katika kituo cha polisi wa utawala mjini Lamu, alimbaka mwanamke huyo wakati akiwa na umri wa miaka 26 usiku wa Desemba 8, 2019, katika nyumba yake iliyoko kwenye makazi ya polisi kituoni.

Mahakama ilielezwa kuwa mwanamke huyo alikuwa amefika kwenye kituo hicho mwendo wa saa mbili za usiku kupiga ripoti kwamba mumewe alikuwa akimlazimisha kuavya mimba.

Muda mfupi baada ya mwanamke huyo kuondoka kituoni, mshukiwa anadaiwa kumfuata nyuma, ambapo alimsimamisha na kumwahidi kwamba angemsaidia kupata haki katika kesi dhidi ya mumewe.

Wakati wa mazungumzo hayo, mvua ilianza kunyesha, ambapo Bw Ouma alimuomba mlalamishi waingie kwenye nyumba yake iliyoko makazi ya polisi.

Muda mfupi baada ya kuingia nyumbani humo, Bw Ouma alifunga mlango kwa ndani na kisha kumpokonya simu mlalamishi na kuizima.

Alimbaka mwanamke huyo kwa muda wa saa moja kabla ya mlalamishi kupata mwanya baadaye na kutorokea nyumba ya jirani yake, na kuacha funguo za nyumba yake pamoja na handibegi ndani ya chumba cha polisi huyo.

Siku iliyofuata, mlalamishi aliripoti yaliyotokea, hatua iliyosababisha konstebo huyo wa polisi kukamatwa na kufunguliwa mashtaka.

Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Lamu, Allan Temba, alisema upande wa mashtaka ulidhihirisha kuwa mshukiwa na makosa.

Mahakama pia ilimpata na hatia ya kutumia mamlaka yake kama polisi kumdhulumu mwanamke huyo kwa kumlazimisha kushiriki ngono naye.

Hukumu itatolewa Ijumaa.

  • Tags

You can share this post!

Fujo msanii stadi akizikwa

Mwandani mwingine wa Ruto amulikwa

adminleo