Sergio Ramos afunga penalti kusaidia Real Madrid kufungua pengo la pointi nne kati yao na Barcelona kileleni mwa jedwali
Na CHRIS ADUNGO
PENALTI iliyochanjwa na beki Sergio Ramos katika dakika ya 79 iliwawezesha Real Madrid kusajili ushindi wa 1-0 dhidi ya Getafe mnamo Julai 2, 2020 na kufungua pengo la alama nne kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).
Hadi beki Mathias Olivera wa Getafe alipomchezea Dani Carvajal visivyo ndani ya msambamba na kuchangia penalti, dalili zote ziliashiria kwamba Real wangalilazimishiwa sare tasa katika mechi hiyo iliyochezewa uwanjani Alfredo di Stefano.
Penalti hiyo ilikuwa ya 21 kwa nahodha Ramos kupiga akivalia jezi za Real.
Getafe ambao wanapigania nafasi ya kunogesha kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao walianza mechi dhidi ya Real kwa hamasa kubwa huku kipa Thibaut Courtois akilazimika kupangua makombora matano aliyoelekezewa na wavamizi wa Getafe chini ya dakika 15 za ufunguzi wa kipindi cha kwanza.
Gozi hilo lilitawaliwa na hisia na makabiliano makali huku jumla ya wachezaji 10 wakionyeshwa kadi za manjano.
Real walionekana kulemewa kabisa na wageni wao huku majaribio yao mawili pekee langoni pa Getafe kabla ya penalti iliyofungwa na Ramos yakitokana na juhudi za kiungo Luka Modric na mshambuliaji Karim Benzema.
Chini ya kocha Zinedine Zidane, Real kwa sasa wanahitaji kusajili ushindi katika mechi nne kati ya tano zilizosalia katika kampeni za La Liga msimu huu ili kuwapiga kumbo mabingwa watetezi Barcelona na kutia kapuni taji lao la kwanza la soka ya Uhispania tangu 2012.
Real kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 74, nne zaidi kuliko Barcelona waliolazimishiwa sare ya 2-2 kutoka kwa Atletico Madrid katika mchuano wao wa mwisho.
Baada ya kuvaana na Athletic Bilbao mnamo Julai 5, 2020, Real wamepangiwa kupepetana na Alaves, Granada, Villarreal na Legane mtawalia. Kwa upande wao, Barcelona wameratibiwa kuchuana na Villarreal mnamo Julai 5 uwanjani Estadio de la Ceramica kabla ya kushuka dimbani kukabiliana na Espanyol, Real Valladolid, Osasuna na Alaves kwa usanjari huo.
Atletico wanashikilia nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 59, saba zaidi kuliko Getafe wanaofunga mduara wa sita bora nyuma ya Sevilla na Villarreal wanaojivunia alama 57 na 54 mtawalia.
MATOKEO YA LA LIGA (Julai 2, 2020):
Real Madrid 1-0 Getafe
Eibar 0-2 Osasuna
Sociedad 2-1 Espanyol