Habari Mseto

Wafanyakazi saba wa Lamu Palace wawekwa karantini hotelini humo

July 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na KALUME KAZUNGU

WAFANYAKAZI saba wa hoteli ya kifahari ya Lamu Palace iliyoko kisiwa cha Lamu wamewekwa kwenye karantini ya lazima.

Hii ni baada ya mmoja wa wahudumu wa hoteli hiyo kuwa miongoni mwa watu wawili waliopatilana wakiugua Covid-19 Jumapili.

Akithibitisha, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia, amesema waliafikia kuwatenga wafanyakazi hao ndani ya hoteli yao kwa siku 14 ili kuzuia uwezekano wa kueneza Covid-19 endapo watakuwa tayari wameambukizwa na mwenzao aliyepatikana na maradhi hayo.

Bw Macharia amesema kutengwa kwa saba hao ni hatua ya tahadhari kama inavyoshauriwa na Wizara ya Afya nchini.

“Tumeamua kuwatenga wafanyakazi saba wa hoteli ya Lamu Palace kwa siku 14 kama tahadhari ili kuzuia kuenea kwa Covid-19 endapo aliyepatikana na maradhi hayo atakuwa tayari amewaambukiza wafanyakazi wenzake,” akasema Bw Macharia.

Naye Waziri wa Afya katika serikali ya Kaunti ya Lamu, Dkt Anne Gathoni amesema tayari wamechukua sampuli kutoka kwa saba hao na kuzisafirisha katika Maabara ya Taasisi ya Utafiti wa Matibabu (Kemri) eneo la Kilifi.

Amesema timu ya wataalamu wa afya pia inaendeleza harakati za kuwasaka watu zaidi ambao huenda walitangamana na wagonjwa wawili wa Covid-19, Kaunti ya Lamu.

Amewataka wananchi kuwa waangalifu na kutii maelekezo yote yanayotolewa na Wizara ya Afya nchini ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

“Tayari tumechukua sampuli kutoka kwa wafanyikazi hao saba wa Lamu Palace. Tumepeleka sampuli hizo Kilifi kwa upimaji. Pia tunaendeleza shughuli ya kuwatafuta watu zaidi ambao huenda walitangamana na wagonjwa wawili wa Covid-19 walioko Lamu,” akasema Dkt Gathoni.