• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:45 PM
FATAKI: Ni unafiki kukejeli wanawake waliokataa kutumia ‘rasilimali’

FATAKI: Ni unafiki kukejeli wanawake waliokataa kutumia ‘rasilimali’

Na PAULINE ONGAJI

PENGINE umekutana na picha fulani mtandaoni inayoonyesha mabinti wawili wakining’inia nyuma ya lori.

Japo haijulikani picha hiyo ilitoka wapi na ilipigwa lini, ilichochea maoni mengi mtandaoni hasa miongoni mwa akina kaka.

Kuna baadhi ya watu waliohuzunishwa na picha hiyo ambayo bila shaka iliakisi hali ngumu ya kiuchumi inayoshuhudiwa kwa sasa, lakini kwa wengine, hii ilikuwa fursa ya kuwakejeli mabinti hao na wanawake kwa jumla.

“Mambo yamekuwa magumu kiasi cha kwamba sasa ma slay queen wanadandia malori,” kaka mmoja alisema.

Inashangaza kwamba katika jamii inayosisitiza umuhimu wa mwanamke kujitafutia badala ya kutegemea misaada kutoka kwa wanaume, kuna watu walio na ujasiri wa kuwakejeli na kuwatusi mabinti wawili walioweka aibu kando, na kutumia mbinu ya usafiri isiyowatia kwenye hatari ya kutumia uke wao kujinufaisha.

Na nina uhakika kwamba iwapo wangeomba lifti kisha wakumbane na hatari au mauti, wengi wangekuwa mstari wa mbele kufoka jinsi mabinti wanavyofurahia vitu vya bwerere.

Hii yanikumbusha chapisho fulani la utani mtandaoni ambapo kuna jamaa fulani aliyekuwa akimuomba Rais kuongeza muda wa kafyu wakati huu wa virusi vya corona ili hali ngumu ya maisha iwalazimu ma-slay-queen kuanza kufanya vibarua vya mjengo.

Matamshi haya yanaakisi jinsi jamii ilivyo tayari kumdhihaki mwanamke aliyeweka ujinsia wake kando na kutia bidii ili kujipatia riziki, na wakati huo huo imejiandaa kumkashifu yule aliyeamua kutochoka, na badala yake anatumia ‘rasilimali’ aliyopewa na Mungu kupata anachohitaji bila jasho.

Ni mara ngapi umeshuhudia mwanamke akikejeliwa kwa kufanya kazi ambayo kidogo inaonekana kupunguza sifa zake za kike?

Kwa mfano, akifanya kazi inayohusisha kugusa uchafu kama vile kuuza makaa, anachekwa na kukashifiwa kwa kutojishughulikia.

Akiamua kufanya kazi ya nguvu inayopunguza “sifa za uke” kwenye baadhi ya sehemu zake za mwili, anaitwa mwanamume.

Nakumbuka kaka mmoja aliyemdhihaki binti fulani aliyekuwa akifanya kibarua cha kuuza maji mtaani kwa kutumia mkokoteni, na kusema kwamba mikono yake ilikuwa migumu kama ya mwanamume.

Huu ni unafiki wa hali ya juu kuwakejeli akina dada wanaoweka ujinsia wao kando, na kung’ang’ana sawa na wanaume.

 

[email protected]

You can share this post!

FUNGUKA: ‘Ukija kwangu nguo ziache mlangoni!’

CHOCHEO: Mfadhaiko wa corona wafanya miereka ya kitandani...

adminleo