Makala

UMBEA: Unavyoweza kukabili huzuni ya kuondokewa na umpendaye

July 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SIZARINA HAMISI

MAISHA ni safari ndefu.

Katika harakati za maisha huwa tunakutana na misiba, maombolezo na wakati mwingine matukio ya kukatisha tamaa.

Wengi wetu tunapokutana na hali hizo huwa tunashikwa na kigugumizi na kupata utata jinsi ya kusuluhisha.

Hivi karibuni nilihudhuria matanga ya rafiki yangu ambaye alipoteza maisha yake ghafla na kuacha mume na watoto ambao bado ni wadogo.

Hakuna mjuaji wala mtaalam kwenye suala la kufiwa, na hata mume wa huyu rafiki yangu ambaye amebaki na watoto wawili walio chini ya umri wa miaka 12 alinieleza jinsi ambavyo anahisi dunia imemuinamia.

Akanieleza kwamba uchungu anaohisi, hawezi kuueleza na hajui jinsi gani ataishi na watoto ambao muda mwingi walikuwa wakitunzwa na kuangaliwa na marehemu mkewe.

Wakati akiendelea kuzungumza nami, wakatokea wanaume rafiki zake na kumsalimia, kumpa pole na kumwambia ajikaze, kwani yeye ni mwanamume.

“Watoto wanakuangalia, jipige moyo konde na vumilia, huo ndio uanaume.”

Sikutia neno, bali walipoondoka, akatingisha kichwa na kuniambia jinsi ambavyo kila mtu anataka aonyeshe uanaume wake, wakati moyo wake umevurugika na hana nguvu hata ya kuangalia kesho itakuwaje.

Kwa wasioelewa, unapoondokewa na mtu ama kitu unachokipenda sana, inachukua hatua ili kuweza kurudia tena hali ya awali.

Maombolezo yana hatua ambazo hazitakiwi kuharakishwa, bali kutambuliwa na kukubaliwa na mhusika na wale walio karibu naye.

Maombolezo ni hisia unazopata pale unapofiwa na mtu wa karibu yako, ama uliyekuwa unampenda na labda aliyekuwa sehemu ya maisha yako.

Maumivu haya huwa hayaelezeki, kwani hakuna aliyewahi kuyasimulia yakaeleweka kwa asiyeyahisi. Kwani huwa na mchanganyiko wa hasira, kushindwa kuamini, kujihisi mkosefu na huzuni iliyopitiliza.

Maumivu haya ya kuondokewa na mtu aliye karibu nawe yanaweza kuathiri afya ya muombelezaji na kusababisha akashindwa kulala vizuri, akashindwa kula na hata kuwa na fikra sahihi.

Haya yote ni hatua za kawaida za kuombeleza pale unapofiwa. Changamoto wanayoipata wengi ni jinsi ya kuhisi maumivu haya, kuyakubali na kuelewa jinsi ya kuishi nayo na kuyamaliza salama.

Maumivu ya maombolezo sio lazima yawe ni kufiwa, inawezekana ikawa ni kuachana na umpendaye, kupoteza kazi ama biashara, kupoteza uwezo wa kukidhi mahitaji ya familia, kustaafu, kuvunjika kwa urafiki ama kuuguliwa na mtu wa karibu.

Kwa lolote litakalokutokea kwa kumpoteza mtu, kitu ama uhusiano, utambue kwamba hisia za maombelezo ni kawaida na ni suala lako binafsi. Usihisi aibu kwa jinsi unavyojisikia, kwani maombelezo ni suala binafsi, halina utaratibu muafaka.