• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
Ronaldo afunga frikiki na kuweka rekodi ya utitigaji nyavu kambini mwa Juventus

Ronaldo afunga frikiki na kuweka rekodi ya utitigaji nyavu kambini mwa Juventus

Na CHRIS ADUNGO

CRISTANO Ronaldo alifunga bao kupitia mpira wa ikabu (frikiki) katika jaribio lake la 43 akiwa ndani ya jezi za Juventus waliowapokeza Torino kichapo cha 4-1 katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Bao la Ronaldo lilimwezesha kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza tangu 1961 kuwahi kufunga mabao 25 kambini mwa Juventus katika kipindi cha msimu mmoja wa Serie A.

Gozi kati ya Juventus na Torino lilimpa kipa mkongwe Gianluigi Buffon fursa ya kuweka rekodi ya mchezaji aliyewahi kuwajibishwa katika michuano mingi zaidi katika historia ya Serie A.

Kufikia sasa, mlinda-lango huyo aliyerefusha mkataba wake kambini mwa Juventus kwa mwaka mmoja zaidi mnamo Juni 29, amechezeshwa mara 648 katika Ligi Kuu ya Italia.

Paulo Dybala aliwafungulia Juventus karamu ya mabao kunako dakika ya tatu kabla ya Ronaldo kumega krosi safi iliyokamilishwa na Juan Cuadrado katika dakika ya 29.

Andrea Belotti alifunga bao la Torino mwishoni mwa kipindi cha kwanza kabla ya Ronaldo kucheka na nyavu za wageni wao waliojifunga mwishoni mwa kipindi cha pili kupitia kwa Levy Koffi Djidji.

Ronaldo kwa sasa anajivunia kufunga mabao 46 kupitia frikiki katika kiwango cha soka ya klabu. Alifunga mabao 32 kati ya hayo akiwa mchezaji wa Real Madrid na 13 akivalia jezi za Manchester United.

Anakuwa mchezaji wa kwanza wa Juventus kufunga mabao 25 katika msimu mmoja tangu Omar Sivori aweke rekodi hiyo mnamo 1960-61. Zikisalia mechi nane zaidi kabla ya kivumbi cha Serie A kutamatika rasmi muhula huu, Ronaldo anapigiwa upatu wa kuivunja rekodi hiyo ya Sivori.

Mechi ya 648 ya Buffon, 42, ilimwezesha kuvunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na beki wa zamani wa AC Milan, Paolo Maldini.

Baada ya kuwajibishwa na Paris Saint-Germain (PSG) mara 17 katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) msimu uliopita wa 2018-19, Buffon kwa sasa anashikilia rekodi ya mchezaji aliyewajibishwa mara nyingi zaidi katika soka ya bara Ulaya (mechi 665).

Gareth Barry, ambaye kwa sasa huvalia jezi za West Bromwich Albion katika Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Uingereza (Championship) aliwahi kupiga jumla ya mechi 653 katika soka ya EPL.

Juventus ambao wanafukuzia taji lao la tisa mfululizo katika Serie A, kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 75, saba zaidi kuliko nambari mbili Lazio.

You can share this post!

Vita vilivyotokea katika Seneti Jumatano vinachunguzwa,...

Saka, Lacazette wasaidia Arsenal kupepeta Wolves ligini

adminleo