• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Bayern Munich wapepeta Bayer Leverkusen 4-2 kujizolea taji la 20 la German Cup

Bayern Munich wapepeta Bayer Leverkusen 4-2 kujizolea taji la 20 la German Cup

Na CHRIS ADUNGO

ROBERT Lewandowski alihakikisha kwamba anafunga zaidi ya mabao 50 msimu huu kwa kucheka na nyavu za Bayer Leverkusen mara mbili na kusaidia Bayern Munich kusajili ushindi wa 4-2 uliowazolea taji la 20 la German Cup mnamo Julai 4, 2020.

Huu ni msimu wa 13 kwa Bayern ambao pia ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kutia kapuni jumla ya mawili katika msimu mmoja.

Frikiki ya David Alaba iliwaweka Bayern kifua mbele kunako dakika ya 16 kabla ya fowadi wa zamani wa Arsenal, Serge Gnabry kufunga la pili dakika nane baadaye katika uwanja mtupu wa Olympic jijini Berlin.

Lewandowski ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Poland, alivurumisha kombora zito langoni pa Leverkusen katika dakika ya 59 na kumwacha hoi kipa mzawa wa Slovakia na raia wa Finland, Lukas Hradecky.

Ingawa Sven Bender alipania kurejesha Leverkusen mchezoni katika dakika ya 63, juhudi zake zilizimwa na Lewandowski aliyefunga bao lake la pili kunako dakika ya 89, sekunde chache kabla ya wapinzani wao kupata penalti iliyojazwa kimiani na Kai Havertz anayewaniwa pakubwa na Chelsea, Juventus na Liverpool.

Bayern kwa sasa wameweka rekodi mpya katika soka ya Ujerumani baada ya kusakata jumla ya mechi 26 bila ya kupoteza na kuambulia sare moja pekee tangu Disemba 2019 chini ya kocha Hansi Flick.

Ufanisi wao wa kusajili ushindi katika jumla ya mechi 17 mfululizo pia ni rekodi mpya katika historia ya soka ya Ujerumani.

Ingawa Leverkusen walianza mchezo kwa matao ya juu na kwa wakati fulani kuonekana kuwazidi maarifa wapinzani wao katika takriban kila idara, Bayern waliwasoma vyema katika dakika 15 za kwanza za mchezo na kuwapiku kwa ujanja.

Hadi kufikia sasa msimu huu, Lewandowski anajivunia jumla ya mabao 51 kutokana na mechi 44 ambazo amewasakatia Bayern ambao bado wanafukuzia ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA). Wanajiandaa kurudiana na Chelsea katika mkondo wa pili wa hatua ya 16-bora mwezi ujao baada ya kusajili ushindi wa 3-0 katika mkondo wa kwanza uwanjani Stamford Bridge mnamo Februari 25, 2020.

Tangu kujizolea taji la Uefa Cup mnamo 1988 na German Cup mnamo 1993, Leverkusen wamezidiwa maarifa katika fainali ya UEFA mara moja, mara tatu katika fainali ya German Cup na kuambulia nafasi ya pili katika kivumbi cha Bundesliga mara tano.

Leverkusen wangali na matumaini ya kunyanyua taji la Europa League msimu huu. Watarudiana na Rangers FC mwezi ujao katika hatua ya 16-bora ya kipute hicho wakijivunia ushindi wa 3-1 katika mchuano wa mkondo wa kwanza uliowakutanisha uwanjani Ibrox Arena, Scotland mnamo Machi 12, 2020.

You can share this post!

Saka, Lacazette wasaidia Arsenal kupepeta Wolves ligini

Presha yapanda kambi ya Ruto

adminleo