LA LIGA: Sergio Ramos afunga penalti kindumbwendumbwe dhidi ya Athletic Bilbao na kufanya Real Madrid kunusia ubingwa
Na CHRIS ADUNGO
BEKI na nahodha Sergio Ramos alifungia Real Madrid bao la pekee na la ushindi kupitia penalti kwa mara ya pili mfululizo na kusaidia waajiri wake hao kuwabwaga Athletic Bilbao katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).
Ushindi huo wa Real uliwawezesha kupaa zaidi kwenye msimamo wa jedwali kwa kufungua pengo la alama saba kati yao na Barcelona watakaokutana na Villarreal baadaye usiku wa Julai 5, 2020 uwanjani De la Ceramica.
Ramos alifunga penalti kwa mtindo sawa alioutumia dhidi ya Getafe mnamo Julai 2, 2020 uwanjani Alfredo Di Stefano. Penalti dhidi ya Bilbao ilikuwa zao la tukio la beki mzawa wa Brazil, Marcelo Vieira kuchezewa visivyo na Dani Garcia kunako dakika ya 72. Tukio hilo lilithibitishwa na refa kwa kurejelea teknolojia ya VAR.
Ramos kwa sasa anajivunia kufungia Real jumla ya mabao matano kutokana na mechi saba zilizopita. Real wamesajili ushindi katika mechi hizo zote tano tangu kurejelewa kwa soka ya La Liga.
Mechi kati ya Real na Bilbao ilishuhudia makipa wa pande zote mbili wakisalia bila kibarua cha kufanya kwa takriban dakika zote 90 za mchezo, huku kipa Thibaut Courtois wa Real akielekezewa kombora moja pekee katika kipindi cha kwanza.
Chini ya kocha Zinedine Zidane, Real kwa sasa wanahitaji kusajili ushindi kutokana na mechi tatu pekee kati ya nne zilizosalia ili kutawazwa mabingwa wa La Liga kwa mara ya kwanza tangu 2012.