Michezo

Matumaini ya Barca kunolewa na Xavi yafifia

July 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

BARCELONA wamekabiliwa na pigo baada ya kiungo wao wa zamani, Xavi Hernandez, 40, aliyetarajiwa kupokezwa mikoba ya ukocha, kurefusha mkataba wake kambini mwa Al-Sadd nchini Qatar hadi mwaka wa 2021.

Xavi aliyechezea Barcelona kati ya 1997 na 2015, alikuwa akihusishwa na uwezekano mkubwa wa kurejea uwanjani Camp Nou kudhibiti mikoba ambayo dalili zote zinaashiria kwamba mkufunzi Quique Setien atapokonywa mwishoni mwa msimu huu.

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania, Xavi alikuwa pua na mdomo kukubali mikoba ya Barcelona kwa ahadi ya kulipwa mshahara wa hadi Sh756 milioni kwa mwaka.

Maagano hayo kati ya Xavi na Barcelona yalikuwa yamepigwa mhuri na mshambuliaji Lionel Messi na wanasoka wengine wa haiba kubwa kambini mwa kikosi hicho cha jiji la Catalonia, wakiwemo Gerrard Pique na Sergio Busquets.

Barcelona kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili nyuma ya Real Madrid kwenye jedwali la La Liga huku mizozo ya mara kwa mara kati ya wachezaji na benchi ya kiufundi ikiripotiwa.

Licha ya kuaminiwa kuwa mrithi wa Ernesto Valverde mnamo Januari 2020, presha inaelekea kumzidi nguvu Setien, 61.

Xavi amekuwa kocha wa Al-Sadd tangu mwanzoni mwa msimu huu wa 2019-20 na amesaidia kikosi hicho kunyanyua mataji ya Super Cup na Qatar Cup.

Kiini cha Barcelona kuanza kumvizia kwa minajili ya ukufunzi ni ungamo lake la hivi karibuni kwamba kubwa zaidi katika matamanio yake ni kuwa kocha wa miamba hao kwa azma ya kuwarejeshea uthabiti waliojivunia katika miaka ya awali.