• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
Man United yaisifu Arsenal kutia adabu Wolves

Man United yaisifu Arsenal kutia adabu Wolves

Na CHRIS ADUNGO

USHINDI wa 2-0 uliosajiliwa na Arsenal dhidi ya Wolverhampton Wanderers katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumamosi uwanjani Molineux ulikuwa msaada mkubwa kwa watani wao wa tangu jadi, Manchester United.

Ni matokeo yaliyoibua msisimko wa nadra miongoni mwa mashabiki wa Man-United ambao kwa sasa wameanza kunusia uwezekano wa kufuzu kwa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Man-United waliowapepeta Bournemouth 5-2 katika mechi nyingine mnamo Jumamosi, kwa sasa wanashikilia nafasi ya tano jedwalini kwa alama 55, mbili pekee nyuma ya Chelsea wanaofunga orodha ya nne-bora.

Kikubwa zaidi kinachowaaminisha Man-United kuwa watafuzu kwa kipute cha UEFA muhula ujao, ni uzito wa kibarua kilichopo mbele ya Chelsea.

Baada ya kuvaana na Crystal Palace, Sheffield United na Norwich City kwa usanjari huo, Chelsea watakuwa na mtihani mgumu dhidi ya Liverpool na Wolves katika michuano yao miwili ya mwisho. Mechi hizi za mwisho zitapigwa baada ya Chelsea kupimana ubabe na Man-United katika nusu-fainali ya Kombe la FA uwanjani Wembley mnamo Julai 19.

Kwa upande wao, Man-United wana mteremko mkubwa katika mechi tano zilizosalia katika EPL msimu huu. Baada ya kukabiliana na Aston Villa, Southampton na Palace, watamenyana na West Ham United kabla ya kufunga msimu dhidi ya mabingwa wa 2015-16, Leicester City.

Wolves ambao wamekuwa mwiba kwa miamba wa soka ya Uingereza katika kipindi cha misimu miwili iliyopita, sasa wanashikilia nafasi ya sita kwa alama 52, tatu zaidi kuliko Arsenal ambao wanapigania nafasi za kushiriki Europa League kwa pamoja na Sheffield United, Burnley, Tottenham Hotspur na Everton.

You can share this post!

Matumaini ya Barca kunolewa na Xavi yafifia

Nitachapa kazi na wanaotii amri zangu – Arteta

adminleo