Waumini wasizidi 100 makanisani – Uhuru
Na SAMMY WAWERU
Rais Uhuru Kenyatta Jumatatu ametangaza kwamba maeneo ya kuabudu, ndiyo makanisa na misikiti, yatafunguliwa kwa awamu.
Kufuatia mlipuko wa Homa ya corona nchini Machi 2020, makongamano na mikusanyiko ya umma, iliyojumuisha maeneo ya kuabudu ilipigwa marufuku kwa muda ili kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.
Rais Kenyatta amesema maeneo ya kuabudu yatafunguliwa kwa awamu na kwa kuzingatia sheria na mikakati iliyowekwa kuzuia msambao wa Covid – 19, ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona.
Alisema uamuzi huo, umeafikiwa kufuatia mashauriano kati ya serikali na baraza maalum la baadhi ya viongozi wa madhehebu walioteuliwa kutathmini namna ya kuyafungua, linaloongozwa na Askofu wa Kanisa la Katoliki Dayosisi ya Nyeri Antony Muheria.
Kwenye hotuba yake kwa taifa, Rais Kenyatta alisema baraza hilo limewasilisha ripoti ya sheria na mikakati itakayozingatiwa na madhehebu ya kidini katika ufunguzi wa maeneo ya kuabudu.
“Miongoni mwa ripoti ya mikakati niliyopokea kutoka kwa baraza hilo hii leo (Jumatatu), eneo la kuabudu washirika wasiozidi 100 pekee ndio wataruhusiwa kukongamana,” alisema.
Aidha, baraza hilo limependekeza ibada ya misa iendeshwe kwa muda usiozidi saa moja.
Isitoshe, Rais Kenyatta alisema watakaohudhuria kulishwa chakula cha kiroho ni walio na umri kati ya miaka 13 – 58, huku wenye matatizo tofauti ya kiafya wakihimizwa kusalia nyumbani.
“Mafunzo ya kidini kwa watoto kanisani na katika madrasa yangali marufuku hadi notisi itakapotolewa,” kiongozi wa nchi akaeleza.
Ili kufunguliwa kwa maeneo ya kuabudu, alisema ripoti ya baraza hilo itasambazwa kwa maeneo yote ya kuabudu nchini.
Afueni hiyo kwa makanisa na misikiti inajiri, huku ikibainika baadhi ya washirika wamekuwa wakikongamana kisiri kulishwa chakula cha kiroho.
Marufuku ya mikusanyiko mingine ya umma, imeongezewa muda wa siku 30 zaidi.