Makala

WANGARI: Corona imechangia katika ukuaji wa biashara kidijitali

July 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

IKIWA kuna jambo ambalo limejitokeza kutokana na janga la virusi vya corona ni mabadiliko katika namna ya utendakazi pamoja na utoaji huduma mbalimbali.

Sekta ya biashara pia haijanusurika huku gonjwa hilo likitatiza shughuli na kulazimu mashirika kufikiria upya kuhusu wanavyohusiana na wateja wao katika mchakato wa kuuza bidhaa na huduma.

Mfano mzuri ni kuhusu mashirika ya bima ya afya ambayo kwa hakika yamepata fursa ya kipekee kutokana na janga hilo la kiafya.

Ingawa mashirika hayo pia yameathirika kifedha kutokana na kusambaratika kwa mfumo ya uchumi nchini, Covid-19 pia imetoa nafasi kwa biashara za bima ya afya kukua.

Hii ni kwa kuzingatiwa kwamba gonjwa hilo bado halijapata tiba na hivyo basi, litaendelea kuwa tishio la kiafya kwa jamii katika siku nyingi zijazo.

Kutokana na uhalisia huu, mashirika ya bima ya afya yamo mbioni kuimarisha miundomsingi yao ili kuendelea kuwafikia wateja wao na hata kuvutia wengine wapya katika mazingira haya mapya kijamii na kiuchumi.

Mfumo wa kidijitali ambao tayari ulikuwa umeanzishwa na baadhi ya mashirika katika sekta hiyo hata kabla ya kuzuka kwa janga la Covid-19, umechangia pakubwa kuwezesha utoaji huduma za bima ya afya.

Sawa na katika sekta nyinginezo nchini, virusi vya corona, kando na athari zake za kiafya kwa wahasiriwa, limechangia pakubwa kuharakisha mageuzi ya kidijitali na hali si tofauti katika mashirika ya bima ya afya.

Huku athari za kijamii, kiafya na kiuchumi zikizidi kushika kasi kutokana na makali ya gonjwa hili, mageuzi kidijitali katika sekta ya bima ya afya yamepata mwelekeo mpya.

Baadhi ya mashirika hayo sasa yamewezesha shughuli kadhaa kufanyika kirahisi kielektroniki ikiwemo kufanya mikataba ya kimatibabu na wateja.

Hii ni hatua muhimu ambapo wateja sasa wameimarishwa kiasi cha kuweza kufanya maamuzi muhimu kuhusu afya yao, mtindo wa maisha, na hatimaye kuchagua bima inayofaa mitandaoni, pasipo ushawishi kama ilivyokuwa hapo awali.

Ni bayana kuwa mfumo huu mpya wa bima ya afya kidijitali utawawezesha wateja kupata maelezo zaidi, kuchagua mikataba inayowafaa kwa bei wanayoweza kuimudu na muhimu zaidi, kudai malipo kuhusiana na bima walizochukua.

Isitoshe, wateja pia wanaweza kupokea matibabu, dawa na maagizo ya daktari kupitia mifumo ya afya kidijitali kama vile MyDawa, CheckUps na nyinginenzo, pasipo kulazimika kwenda hospitalini.