Endeni sasa mtangatange, Uhuru aambia mawaziri wake
Na VALENTINE OBARA
RAIS Uhuru Kenyatta sasa amewapa rasmi mawaziri wake ruhusa ya kutembelea sehemu zote za nchi kukagua miradi ya maendeleo na kuvumisha misimamo ya serikali yake.
Kazi hii kwa miaka iliyopita ilikuwa ikiendelezwa na Naibu Rais William Ruto, na ndiyo ilimfanya kubandikwa jina ‘Tangatanga’.
Hata hivyo, Rais baadaye alionyesha kutoridhishwa na ziara hizo za naibu wake kwani Dkt Ruto alisemekana kuzitumia kujitafutia umaarufu wa kisiasa akijiandaa kuwania urais 2022. Hii ni licha ya Rais kutaka kampeni za mapema zikomeshwe.
Baadhi ya wakosoaji wake pia walikuwa wakisema alikuwa akizindua miradi hewa bila bajeti.
Jana, Rais aliwaambia maafisa wakuu serikalini wawe wakizuru pembe zote za nchi kukagua miradi na kuwakilisha serikali mashinani.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ikulu, Rais Kenyatta alitaka jukumu hilo litekelezwe na mawaziri kwa ushirikiano wa karibu na manaibu wao na makatibu wa wizara.
Alisema ushirikiano huo utasaidia kukamilisha miradi kwa wakati ufaao na kwa kiwango cha ubora wa hali ya juu.
“Rais alisema miradi yote lazima itekelezwe kwa muda ulioekwa na kwa kutumia bajeti ambazo zilipitishwa. Alisisitiza msimamo wake wa awali kwamba hakuna miradi mipya itaanzishwa bila idhini yake binafsi,” ikasema taarifa.
Mkutano huo uliofanywa kwa njia ya video ulihudhuriwa na mawaziri, manaibu wao na makatibu wa wizara.
Katika siku za hivi majuzi, baadhi ya magavana na wanasiasa wengine wamesikika wakilalamika kuwa maafisa wakuu serikalini wanatumia mamlaka yao kujitafutia umaarufu wa kisiasa.
Hii ni kutokana na kuwa, baadhi ya maafisa hao wakuu hasa mawaziri tayari wameashiria nia ya kuwania nyadhifa za kisiasa ifikapo mwaka wa 2022.
Wakati huo huo, Rais alitaka viongozi serikalini waache uzembe kwani kukamilisha miradi kutatumiwa kama kigezo cha kupima utendakazi.
Duru zimekuwa zikieleza kuhusu matarajio ya kubadili viongozi wakuu serikalini ili kujumuisha wandani wake wapya wa kisiasa, kutoka katika vyama vya ODM, Wiper, KANU na Chama cha Mashinani.