Tangatanga walia kutengwa katika miradi ya maendeleo
Na MWANGI MUIRURI
WABUNGE wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto, wamelalamika wakidai maafisa serikalini wanatumia miradi ya umma kuweka uhasama wa kisiasa.
Mbunge wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro na Bi Alice Wahome kutoka Kandara wamedai kuna njama ya kutumia miradi hiyo ya maendeleo kushawishi wakazi maeneo ya Kati wamwepuke Dkt Ruto.
Hayo yametokea siku moja tu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuwaagiza mawaziri, manaibu wao na makatibu wa wizara waanze kuzuru kila eneo nchini kukagua miradi ili ikamilike kwa muda ufaao.
Wakiongea na Taifa Leo jana, wawili hao walisema hawatakubali miradi ya maendeleo kutumiwa kuendeleza siasa za kuwagawanya wananchi kwani huduma za kiserikali ni haki ya umma.
Waliteta kuwa kamati kuu ya utekelezaji miradi ya kiserikali ikiongozwa na Waziri wa Usalama wa Nchi, Dkt Fred Matiang’i huwa haiwaaliki wafuasi wa Dkt Ruto katika mikutano ya kuratibu maendeleo.
‘Ijumaa iliyopita, kamati hiyo iliwaalika wabunge wa Murang’a katika mkutano Nairobi kujadili miradi ya maendeleo ya kaunti hiyo. Lakini mimi na mwenzangu wa Kandara hatukualikwa,’ akasema Bw Nyoro.
Mikutano sawa na hii iliandaliwa na viongozi wa Magharibi ambao wanaonekana kuegemea upande wa Rais Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, huku wakosoaji wao wakiachwa nje.
Bw Nyoro alidai kamati hiyo inataka kuhadaa wenyeji wa Murang’a kuwa hawana haki ya kutekelezewa maendeleo ikiwa wao ni wafuasi wa Dkt Ruto.
‘Sisi kama watu wa Murang’a ni walipa ushuru na kutekelezewa maendeleo ni haki ya kimsingi wala sio ya kisiasa. Tunafaa tukatae utapeli huo wa kubaguliwa kwa msingi wa imani yetu ya kisiasa,’ akasema.
Kwa upande mwingine, Bi Wahome alisema Rais alichaguliwa sambamba na Dkt Ruto na ndio wakuu wa serikali kwa pamoja.
‘Imekuwaje tunaambiwa tumtenge Dkt Ruto ilhali kisheria wawili hao ndio serikali? Na itakuwaje tena sasa iwe wafuasi wa Dkt Ruto watanyimwa maendeleo ilihali hata wao hutozwa ushuru sawa na hao wengine?’ akahoji Bi Wahome.
Wawili hao walisema kuwa hawatabanduka kutoka ufuasi wa Dkt Ruto wakisisitiza kuwa wengi wa wapiga kura wa Murang’a wamewaagiza wasalie papo hapo.
Walishikilia kuwa kamati ya Dkt Matiangi kuhusu maendeleo inahadaa wapiga kura mashionani kuwa ndiyo inagawa miradio ya kimaendeleo.