Habari Mseto

Familia yateta chifu kuagiza warudishe mahari

July 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MAUREEN ONGALA

FAMILIA katika kijiji cha Muhoni, eneobunge la Ganze imemkashifu chifu wa eneo hilo kwa kuwaagiza kurudisha mahari ya Sh34,000.Familia hiyo imedai chifu wa Ganze, Thaura Mweni alipanga njama na mume wa binti yao kuwahangaisha.

Mnamo Februari, Bi Sanita Kitsao ambaye ni mama wa watoto sita alirudi kwao akidai kupokea vitisho kutoka kwa mume wake.

Kulingana naye, mumewe alimlaumu kuwa mchawi na alipanga kumuua ndipo akaamua kurudi kwao na watoto wake wawili.

“Sitaki kurudi katika ndoa yangu kwa sababu mume wangu anadai nimeingizwa katika kikundi cha wachawi na baadhi ya jamaa zake kwa hivyo anataka kuniua. Pia sitarudisha mahari kwa sababu nimezaa watoto sita na mimi ndiye nimekuwa nikitafutia familia yangu riziki wakati huo wote,” akasema.

Kakake, Bw Lemmy Jefwa alisema chifu aliandaa mikutano mingi kujaribu kuwapatanisha lakini mwanamume akasisitiza arudishiwe pesa alizolipa kama mahari.

Mkutano wa mwisho ulifanywa Ijumaa iliyopita.Alisema waliripoti kuhusu vitisho vya maisha ya dadake kwa kituo cha polisi cha Ganze.

“Ni wazi kuwa chifu ana ubaguzi. Familia inachukulia suala hili kwa uzito. Hatutaki baadaye tuje kusikia dada yetu aliuliwa akimrudia mume wake,” akasema Bw Jefwa.

Hata hivyo, chifu alitetea msimamo wake na kusema ni utamaduni katika jamii za Mijikenda kwamba mahari inastahili kurudishwa wanandoa wakitengana.

Alisema uamuzi wake kuandaa vikao vingi kujaribu kupatanisha wanandoa hao ulikuwa kusudi ili mwanamke husika apate muda wa kuamua kama kweli anataka kuachana na mume wake au atamrudia.

“Mwanamke amekataa kurudi nyumbani kwake. Hatuwezi kuwalazimisha waishi pamoja na desturi ni kuwa anafaa kurudisha mahari ili mume wake aitumie kuoa mke mwingine akipenda, kwani bado angali ni kijana,” akasema Bw Mweni.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Kilifi, Bw James Mugera alisema polisi wanachunguza suala hilo.

Kulingana na Bi Jefwa, mumewe amekuwa akimpiga sana katika ndoa na wakati wote visa hivyo vilikuwa vikitatuliwa kwa mashauriano ya wazazi wake ambao walikuwa wakiwapatanisha.