• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 PM
Korti yarusha Ngilu kwenye kinywa cha mamba

Korti yarusha Ngilu kwenye kinywa cha mamba

Na KITAVI MUTUA

HATIMA ya utawala wa Gavana wa Kitui, Bi Charity Ngilu, sasa imo mikononi mwa madiwani baada ya Mahakama Kuu kukataa kusitisha mchakato wa kumng’oa mamlakani.

Jaji Weldon Korir jana alitupilia mbali ombi la Bi Ngilu kuitaka mahakama kuzima hoja ya kumwondoa mamlakani, iliyowasilishwa na Kiongozi wa Wengi, Bw Peter Kilonzo.

Uamuzi huo sasa umetoa nafasi kwa makabiliano makali kati ya Madiwani wa Chama cha Wiper, ambao ndio wengi katika bunge la Kaunti ya Kitui, na wale wanaoegemea upande wa Bi Ngilu. Chama cha Wiper kinachoongozwa na Bw Kalonzo Musyoka kina madiwani 30 katika bunge hilo lililo na jumla ya madiwani 54.

Kwa upande mwingine, Chama cha Narc kinachoongozwa na Bi Ngilu kina madiwani 12 pekee, lakini wameungana na Jubilee pamoja na vyama vingine vidogo na madiwani huru.

Ili hoja ya kumng’oa gavana mamlakani ipite, itabidi kuungwa mkono na madiwani 36 ambao ni theluthi mbili. Katika uamuzi wake, Jaji Korir alisema ombi la Bi Ngilu halikutoa sababu za kutosha.

Alisema Seneti pekee ndiyo inaweza kuamua ikiwa Bunge la Kaunti liliwashirikisha wananchi ifaavyo kwenye utaratibu huo.

Jaji alisema ingawa mahakama zinapaswa kuingilia kati na kutatua mizozo inayoibuka kati ya taasisi mbalimbali nchini, kuna mipaka ya kikatiba iliyowekwa kwenye majukumu hayo ambayo lazima iiheshimu.

“Ni muhimu kutambua kuwa mchakato wa kumfurusha gavana uongozini ni njia inayotumiwa na bunge la kaunti kutathmini utendakazi na uwajibikaji wa serikali husikai.

Bunge linatekeleza jukumu lake kikatiba,” akasema kwenye agizo hilo.

You can share this post!

Joho na Junet waendea ‘Baba’ Dubai

Kitoweo cha trafiki chamwagwa baada ya vizuizi kuondolewa...

adminleo