TAHARIRI: Serikali isiwaachie wahuni maamuzi
Na MHARIRI
RIPOTI ya kila siku kuhusu maambukizi ya virusi vya corona inaonyesha kuwa idadi sasa imefika watu zaidi ya 10,000 hapa nchini.
Baada ya watu 379 kuambukizwa katika saa 24 tangu tangazo la mwisho siku ya Jumamosi, sasa watu wote waliopata virusi ni 10,015
Hili ni ongezeko la karibu watu 2,000, chini ya wiki moja tangu Rais Uhuru Kenyatta atangaze kufungua miji ya Nairobi, Mombasa na Mandera. Hili ni ongezeko ambalo hata katika miezi miwili ya kwanza hatukuwa tumeifikisha.
Kwa hivyo mtu yeyote anayejali maisha ya wananchi atajiuliza maswali magumu kuhusu kufunguliwa upya kwa nchi. Leo safari za garimoshi (SGR) kati ya Nairobi na Mombasa zinaanza rasmi.
Serikali inasema safari hizo zitadhibitiwa ili watu wasijae asilimia 100. Kile ambacho haijasema ni jinsi gani watu watadhibitiwa kwenye maeneo ya kuingia au kutoka kwenye treni.
Katika vituo vya SGR – Syokimau na Miritini – maeneo ambako wateja husubiri kuingia ndani ya treni ni madogo kiasi kwamba watu hufinyana. Wizara ya Uchukuzi yapaswa kueleza itachukua hatua zipi kupanua maeneo hayo.
Kesho Jumanne, misikiti na makanisa yaanza kufunguliwa kwa umma.
Masharti yaliyotolewa ni kwamba wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 58 na watoto wa chini ya umri wa miaka 13 hawaruhusiwi kuingia kwa ibada. Kwamba waumini wasizidi 100.
Alipokuwa akitangaza kufungua upya nchi, Rais Kenyatta alisema serikali haina maafisa wa kutosha wa usalama watakaofuatilia kama kanuni hizo zinafuatwa au la.
Inatarajiwa kuwa, japokuwa baadhi ya viongozi wa kidini watajaribu kudhibiti watu, kuna wale ambao kwa kutarajia fungu la kumi la kutosha, huenda wakakiuka kanuni hizo.
Tayari watu ambao wamechukua fursa ya kufunguliwa kwa kaunti tatu, wameanza kusafiri na kusababisha ajali za barabarani zinazoendelea kuua watu. Ni jana tu ambapo mama na mwanawe waliuawa katika kaunti ya Nyeri, gari walilokuwa wakisafiria lilipohusika kwenye ajali.
Masuala haya hayawezi kuachwa mikononi mwa wananchi na watu wengine ambao hawaelewi umuhimu wa maisha. Madereva wa magari ya usafiri wa umma na watu wanaojitokeza kwenda mashambani bila kuzingatia usalama wao na watu wao yafaa wadhibitiwe.
Hili ni jukumu ambalo, japokuwa rais alisema ni la watu binafsi, serikali haiwezi kuliachia wahuni.