DIMBA: Kijana Ferran Torres anawindwa kama mpira wa kona!
Na GEOFFREY ANENE
KINDA Ferran Torres ni mchezaji wa klabu ya Valencia nchini Uhispania anayeng’ang’aniwa kama mpira wa kona na kbalu kubwa kubwa za Ulaya, kwa sababu ya talanta yake ya hali ya juu kama winga wa pembeni kulia.
Tetesi zinasema Barcelona, Real Madrid, Chelsea, Manchester United, Liverpool, Tottenham Hotspur na Borussia Dortmund zinamezea mate raia huyu Mhispania.
Mwezi Juni, ripoti nchini Italia zilidai kuwa Juventus pia wako katika vita vya kutwaa huduma za Torres.
Mchezaji huyu anafahamika kwa bidii na ubunifu wake. Ana ustadi wa kudhibiti mpira kwa karibu huku chenga zake za kasi zikimtambulisha kama anayependa kucheza soka isiyobashirika, jambo ambalo huwatia kiwewe wapinzani.
Torres, 20, alizaliwa mjini Valencia, na kulelewa kisoka katika klabu ya Valencia kuanzia mwaka 2006.
Tangu utotoni, kifungua mimba huyu alipenda soka. Alitazama kwenye runinga wachezaji wakitandaza kabumbu na kujaribu kuiga ujuzi waliofanya.
Wazazi wake pia walichangia katika kumwelekeza kwenye soka. Kila mara walimpeleka uwanjani Mestalla kushuhudia mechi za timu ya Valencia.
Alipofikisha umri wa miaka sita baba na mamake waliamua kumtafutia nafasi katika akademia ya Valencia alikopata mwelekeo mzuri.
Torres alienzi kiungo wa Manchester City David Silva ambaye wakati huo alikuwa mmoja wa wachezaji nyota wa Valencia.
Hakutatizika kuingia timu za umri tofauti za Valencia, na muda si muda alipata fursa ya kuvalia jezi ya timu ya pili ya watu wazima akiwa na umri mchanga wa miaka 16 mnamo Oktoba 2016.
Kiwango kizuri cha mchezo pamoja na uthabiti wake zilisukuma Valencia kuongeza kandarasi yake hadi Oktoba 2017, kabla kuiimarisha tena walipomtia katika kikosi cha kwanza mnamo Januari 1, 2018.
Hakusikitisha. Kinda huyu alithibitishia waajiri wake kuwa hawakukosea kuwa na imani naye, kwani alinawiri kila alipopewa fursa ya kushiriki dimba la Copa del Rey, Ligi Kuu ya La Liga na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).
Torres ni Mhispania wa kwanza kupata goli katika UEFA ambaye alizaliwa miaka ya 2000. Alipata ufanisi huo alipochangia bao wakati Valencia ikichabanga Lille ya Ufaransa magoli 4-1 mwezi Novemba 2019.
Bao hilo pia lilimweka juu ya orodha ya wachezaji walio na umri mdogo kuwahi kufungia Valencia katika historia ya UEFA.
Msimu huu wa 2019-2020, Torres amechezeshwa mechi 41 zikiwemo 31 za La Liga. Amechana nyavu mara sita na kumega pasi saba zilizozalisha mabao.
Torres, ambaye kandarasi yake uwanjani Mestalla itakatika Juni 30 mwaka ujao, ana thamani ya Sh6.0 bilioni sokoni.
Valencia inamlipa mshahara wa Sh5.5 milioni kila wiki, ambazo kwa jumla zinatinga Sh282 milioni kwa mwaka.
Ripoti nchini Uhispania zinasema kuwa Valencia iliweka masharti katika kandarasi yake kwamba, timu yoyote itakayomsaini kabla ya kandarasi hiyo kutamatika italazimika kulipa Sh12.1 bilioni ili kinda huyo awe mali yake.
Asipokuwa uwanjani, Torres anapenda kusafiri, michezo ya majini na kujumuika na familia na marafiki. Pia, anapenda maisha ya anasa ikiwemo magari makubwa, kuishi katika majumba ya kifahari, kuenda likizo na kuponda raha maeneo ya burudani.