COVID-19: Shughuli PSC zapunguzwa
Na CHARLES WASONGA
SHUGHULI za utoaji huduma katika Afisi Kuu ya Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) zilipunguzwa kuanzia Jumatatu, Julai 13, 2020, baada ya visa vya maambukizi ya Covid-19 kugunduliwa miongoni mwa wafanyakazi.
Katika barua iliyotumwa kwa wafanyakazi wa tume hiyo na mwenyekiti Stephen K. Kirogo, tume hiyo ilisema imechukua hatua hiyo ili kuzuia kuenea kwa virusi hivyo.
Sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa wafanyakazi 10 zilibainika kuwa na virusi vya corona baada ya shughuli ya upimaji uliofanyiwa wahudumu wa tume hiyo mnamo Julai 1, 2020.
“Kwa hivyo, afisi kuu ya PSC itafungwa kwa siku 14 kuanzia Julai 13 hadi Julai 24. Ni watu wachache zaidi watakaoruhusiwa kuingia katika afisi za PSC huku huduma za dharura zikitolewa kwa njia ya mtandao,” akasema Bw Kirogo.
Wafanyakazi wote wameshauriwa kujitenga nyumbani kwa angalau siku 21.
Kwa muda ambapo afisi hizo zitakuwa zimefungwa, shughuli ya unyunyuziaji dawa za kuua viini itaendeshwa katika jengo la PSC ili liwe pahala salama.
Hatua hii inajiri wakati ambapo visa vya maambukizi ya virusi vya corona vimeendelea kuongezeka nchini kila siku.