• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 AM
Misikiti yakosa kufunguliwa licha ya Uhuru kutoa idhini

Misikiti yakosa kufunguliwa licha ya Uhuru kutoa idhini

WACHIRA MWANGI na MISHI GONGO

WAISLAMU jana Jumanne walisusia kuswali misikitini kutokana na masharti makali yaliyotolewa na serikali pamoja na hofu ya maambukizi.

Ilikuwa ni siku ambayo kamati ya makundi ya kidini ilikuwa imetangaza kuwa maeneo ya ibada yangeanza kufunguliwa.

Mnamo Julai 6, 2020, Rais Uhuru Kenyatta aliagiza maeneo ya ibada yafunguliwe, lakini kwa masharti kwamba maombi yataandaliwa kwa muda wa saa moja na kuhudhuriwa na watu 100 pekee.

Vilevile waumini ambao wana umri wa miaka 58 na zaidi pamoja na watoto wa umri wa miaka 13 na chini waliagizwa wasihudhurie ibada.

Misikiti mingi jijini Mombasa jana Jumanne haikufunguliwa jinsi ilivyotarajiwa.

Baadhi ya misikiti iliyosalia kufungwa ni Masjid Umma Kulthum, Mbaruk, Baluchi, Konzi, Sheikh Jundan na Sakina.

Ni msikiti Musa pekee eneo la Majengo ulioanza ibada hizo, sawa na msikiti mmoja eneo la Eastleigh jijini Nairobi.

Baadhi ya waumini waliokuwa wamejiandaa kushiriki ibada misikitini walipata imefungwa.

“Ninafanya kazi mjini. Nimekuja kuswali lakini nashangaa kuwa bado misikiti haijaruhusu watu kufanya ibada ndani,” akasema Bw Yassir Ali katika msikiti wa Baluchi.

Naye Fatma Imran alisema haelewi ni kwa nini misikiti haijafunguliwa, japo iliruhusiwa kurejelea shughuli zake za kawaida.

Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu (CIPK) lilitoa wito wa kuangazia upya mwongozo wa kufungua sehemu za ibada.

Mwenyekiti wa CIPK, Ustadh Muhmmad Shaaban alipendekeza kwamba muda wa maombi unafaa kuongezwa.

“Suala kuu ni kwamba makanisa na misikiti mingi haiwezi kufunguliwa kwa kuzingatia mwongozo uliotolewa. Muda wa saa moja kwa swala ni mfupi sana. Muda huo unafaa kuongezwa ili waumini waombee nchi,” akasema Ustadh Shaaban.

Msomi huyo wa dini pia alishangaa ni mbinu ipi ambayo itatumika kuhakikisha watu 100 pekee ndio wanahudhuria ibada na kuwaacha nje wengine.

“Tuna misikiti ambayo hata zaidi ya watu 1,000 wanaweza kuswali kwa wakati moja. Takwimu ya watu 100 inafaa kuangaliwa upya na kuongezwa,” akaongeza.

Mkurugenzi wa Elimu wa CIPK, Imamu Zenu Bin Ali Mohamed naye alieleza Taifa Leo kwamba mwongozo wa kufungua misikiti ni mgumu na hauwezi kutimizika.

Viongozi wa wengi wa makanisa pia wamesema hawatafungua maeneo ya ibada wakisema ni vigumu kutekeleza kanuni zilizotolewa na serikali.

You can share this post!

Familia Mombasa yamtafuta mtoto aliyetoweka Jumamosi

TAHARIRI: Wizara ya Afya izuie vifo hivi

adminleo