Michezo

Cameroon yajiondoa kuwa mwenyeji hatua za mwisho kampeni za Klabu Bingwa Afrika

July 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Soka la Afrika (CAF) litalazimika kutafuta mwenyeji mpya wa mechi za hatua za mwisho za kampeni za Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) baada ya Cameroon kujiondoa.

Mnamo Juni 30, 2020, CAF iliteua Cameroon kuandaa mechi tatu zilizosalia katika kampeni za Champions League msimu huu; yaani michuano miwili ya nusu-fainali na fainali mnamo Septemba 2020.

Mechi hizo zilizoahirishwa mnamo Machi 2020 kwa sababu ya janga la corona, zinatazamiwa kushirikisha vikosi vya Al Ahly na Zamalek za Misri na Raja Casablanca na Wydad Casablanca kutoka Morocco.

Seidou Mbombo Njoya ambaye ni Rais wa Shirikisho la Soka la Cameroon amesema kwamba itawawia vigumu kuwa wenyeji wa michuano hiyo baada ya asilimia kubwa ya washikadau, ikiwemo serikali ya Cameroon kufichua hofu ya kuongezeka kwa maambukizi mapya ya ugonjwa wa Covid-19 iwapo wataandaa mashindano hayo.

Al Ahly wanaojivunia kunyanyua taji la CAF Champions League mara nane, wamepangiwa kuvaana na Wydad walioambulia nafasi ya pili msimu uliopita wa 2018-19 huku Raja wakipimana ubabe na Zamalek SC.

CAF ilisema kwamba mechi za nusu-fainali sasa zitakuwa za mkondo mmoja pekee badala ya mikondo miwili kama awali.

Vikosi vitalazimika kupiga mechi kwa dakika 30 za ziada na mshindi kuamuliwa kupitia penalti iwapo vitakuwa vikitoshana nguvu kufikia vipindi vya dakika 90 na 120. Aidha, kila mshiriki atakuwa na idhini ya kuwajibisha hadi wanasoka watano wa akiba badala ya watatu wa kawaida.

Mechi za nusu-fainali na fainali za Kombe la Mashirikisho barani Afrika (CAF Confederations Cup) ambazo kwa sasa zitakuwa za mkondo mmoja pekee msimu huu, zitachezewa nchini Morocco.

Mechi hizo zitashirikisha Pyramids FC (Misri), Horoya Conakry (Guinea), RS Berkane (Morocco) na Hassania Agadir (Morocco).