Michezo

Aduda akana kuwepo kwa muungano mkali wa kumlambisha Mwendwa sakafu uchaguzi ujao wa FKF

July 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

LORDVICK Aduda ambaye ni mwaniaji wa urais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) amekana kuwepo kwa mpango kati yake na baadhi ya wagombezi wengine kuungana ili kumbandua rais wa sasa, Nick Mwendwa kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Aduda na wawaniaji wengine watatu waliandaa kikao cha zaidi ya saa tatu katika hoteli moja jijini Nairobi katika tukio ambalo liliibua tetesi nyingi za kutokota kwa muungano mkubwa utakaomtikisa Mwendwa na hatimaye kumdengua madarakani.

Wagombezi watatu walioshiriki kikao hicho kinachosemekana kuagizwa na Aduda ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor Mahia, ni Nicholas Musonye, Sammy Shollei na Twaha Mbarak.

“Tulikutana tu kama wadau wa soka ili kujadili masuala mbalimbali yanayohusu kandanda ya humu nchini. Hatukujadili mambo mengi kuhusu uchaguzi. Tulikuwa tu wawakilishi wa wadau na wawaniaji wote wengine ambao kwa sababu moja au nyingine hawakuwezeshwa kuhudhuria mkutano. Sina mwao kabisa kuhusu kuwepo kwa njama au mpango wa kuunda muungano. Kila mgombezi anawania urais kivyake na kwa sababu ambazo amewapa wapigakura,” akasema Aduda.

Ingawa hivyo, mnamo Juni 2020, Shollei aliwahi kudokeza mpango wa kuundwa kwa muungano mpya miongoni mwa baadhi ya wawaniaji wa kiti cha urais wa FKF.

Hii ni baada ya Naibu Rais wa zamani wa FKF, Musonye ambaye ni Katibu Mkuu wa zamani wa Cecafa na mwaniaji wa zamani wa urais wa FKF Hussein Mohammed kukutana tena katika hoteli moja jijini Nairobi.

Wakati huo, watatu hao walijadiliana kuhusu uwezekano wa kuungana na wawaniaji Andrew Amukowa wa eneo la Magharibi ya Kenya, Mubarak wa Mombasa na Aduda. Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa AFC Leopards Dan Shikanda, upo mpango wa kushawishi Shollei, Mohammed na wawaniaji wengine kuzima maazimio yao ya kuendea urais wa FKF na badala yake kumwachia Musonye awanie wadhifa huo na washindani wengine kisha wao wajitwalie nafasi nyinginezo katika uongozi ujao wa FKF.

Kwa mujibu wa mikakati na mpangilio mpya wa watatu hao, Mohammed anapigiwa upatu kukiendea kiti cha Afisa Mkuu Mtendaji wa FKF naye Shollei awanie nafasi ya kuwa Naibu Rais.

Uchaguzi huo wa kitaifa wa FKF uliokuwa ufanyike mnamo Machi 2020, kwa sasa umefutiliwa mbali mara mbili huku vinara wa Shirikisho la Soka la Duniani (FIFA) wakipendekeza kuandaliwa kwa mkutano kati yao na Serikali ya Kenya na baadhi ya washikadau wa soka ili kufanikisha uchaguzi utakaotawaliwa na haki na usawa.

Wengine wanaowania urais wa FKF ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya St Peter’s Mumias Cosmas Nabongolo, aliyekuwa Mwenyekiti wa FKF Sam Nyamweya, Mwenyekiti wa zamani wa Leopards Alex Ole Magelo, Gavana wa zamani wa Kaunti ya Vihiga Moses Akaranga, Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa FKF Herbert Mwachiro na mwanachama wa zamani wa Kamati Kuu ya FKF tawi la Nyanza, Tom Alila.