Twapotoshwa kuhusu corona?

WANDERI KAMAU na ANGELA OKETCH

HALI ya wasiwasi imeibuka nchini kuhusu ukweli wa vipimo vya virusi vya corona baada ya maabara mbili tofauti kutoa matokeo yanayotofautiana.

Hii ilizuka baada ya wafanyakazi 17 wa Shule ya St Andrew’s Turi iliyo katika Kauti ya Nakuru kupimwa katika maabara ya Lancet na matokeo yakaonyesha wana corona, kabla ya Taasisi ya Utafiti wa Kimatibabu ya Kenya (Kemri) kutoa yake yaliyoonyesha hakuna aliyeambukizwa.

Kwenye uchunguzi wa kwanza uliofanywa na Lancet, sampuli 24 zilichukuliwa katika taasisi hiyo na matokeo yakaonyesha kuwa wafanyakazi 17 kati yao walikuwa wakiugua Covid-19.

Hata hivyo, hali iligeuka baada ya shule hiyo kupeleka sampuli hizo hizo kwa Kemri, ambapo matokeo yalionyesha hakuna hata mtu mmoja aliyekuwa ameambukizwa.

Hali hiyo imeibua maswali kuhusu matokeo ya Covid-19 yanayotolewa nchini na ikiwa Wakenya wanapaswa kuendelea kuyaamini, ikizingatiwa hii si mara ya kwanza kwa matokeo kutofautiana, licha ya sampuli zilizopimwa kuwa sawa.

Mnamo Juni 8, Bi Khalid Nafula alithibitishwa kuambukizwa corona baada ya sampuli zake kupimwa na Lancet, lakini baada ya kupimwa na Kemri ilibainika hakuwa na virusi.

Hii inaibua maswali kuhusu ni Wakenya wangapi wamepewa matokeo yasiyo ya kweli, wangapi wamo karantini ama hospitali kwa kupimwa vibaya na iwapo takwimu zinazotolewa na serikali kila siku ni za ukweli ama zinapotosha.

Hata hivyo, Afisa Mkuu Mtendaji wa Lancet katika eneo la Afrika Mashariki, Dkt Ahmed Kalebi anasema kuwa ni kawaida kwa matokeo kutofautiana.

Wasiwasi pia umesababishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa kuendelea kutoa taarifa zinazokanganya kuhusu Covid-19.

Juni 2020 WHO ilikanganya ilipotoa ripoti kuwa watu walioambukizwa corona lakini hawana dalili hawawezi kusambaza virusi hivyo kwa wengine.

Hii ni kinyume na kauli ambayo imekuwa ikitolewa na maafisa wa afya wa Kenya kuwa watu wasio na dalili ndio wanasambaza virusi hivyo nchini. Asilimia 78 ya Wakenya waliothibitishwa kuwa na Covid-19 hawana dalili zozote.

Pia kumekuwa na hali ya kukanganya kuhusu jinsi virusi hivyo vinavyoenea, baada ya uchunguzi wa majuzi wa Taasisi ya Kuzuia Magonjwa (CDC) nchini Amerika kusema kuna uwezekano wa corona kusambazwa kupitia hewa.

Awali, WHO na maafisa wa afya wamekuwa wakisisitiza virusi hivyo vinasambazwa kupitia sakafu ama kukaribia mtu anayekohoa, kupiga chafya ama kutoa makamasi wala sio hewani.

Mnamo Aprili, WHO ilisema kuwa watu ambao hali zao za afya ni nzuri hawafai kuvaa barakoa, kwani wako salama hata bila kuzivaa, huku mataifa mbalimbali ikiwemo Kenya yakisisitiza lazima kila mtu avae barakoa anapokuwa maeneo ya umma.

Kulingana na WHO, uvaaji barakoa unawapa watu imani ya uwongo kuwa hawawezi kuambukizwa, hivyo kupuuzilia mbali kanuni zingine muhimu kama kuosha mikono, kujitenga na kutotangamana na watu wengi.

“Barakoa zinapaswa kuachiwa watu ambao tayari wamethibitishwa kuambukizwa corona au wanatangamana kwa karibu na watu walioambukizwa. Hilo linajumuisha wahudumu wa afya na wale wanaowashughulikia majumbani mwao,” likaeleza.

Suala la ubora wa barakoa pia linakanganya Wakenya kwani kumekuwa na maski za kila aina, zingine zikisemekana kuwa hazina uwezo wa kukinga mtu kuambukizwa kwani nyingi zinatengenezwa kiholela bila uangalizi wa serikali.

WHO ilisema ni jukumu la nchi husika kuhakikisha kuwa barakoa zinazotengenezwa na viwanda mbalimbali ni za hali ya juu.

Hata hivyo, msimamo wa WHO umekosolewa na baadhi ya wataalamu wanaoshikilia kuwa uvaaji barakoa unapunguza uwezekano wa mtu kuambukizwa.

Hapo Jumatano, Shirika la Amerika la Kuzuia Magonjwa (CDC) lilitoa taarifa likiwashauri watu kuvaa barakoa kama njia ya kuzuia maambukizi.

Habari zinazohusiana na hii