Jinsi Sonko alivyotaka aelezwe ikiwa kuna baa yenye shughuli katika majengo ya bunge
Na CHARLES WASONGA
GAVANA wa Nairobi Mike Sonko aliibua kicheko alipofika mbele ya maseneta kwa kuuliza ilipo baa alipoalikwa kwa chakula cha mchana katika majengo ya bunge.
Sonko alikuwa amefika mbele ya kamati ya seneti kuhusu uhasibu (CPAIC) kujibu maswali yaliyoibuliwa katika ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Umma katika miaka ya kifedha ya 2015/2016, 2016/2017 na 2017/2018.
Hata hivyo, aliiambia kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Kisii Sam Ongeri kwamba hangeweza kuwasilisha stakabadhi husika za matumizi ya fedha kwa sababu amezuiwa na mahakama kuingia ofisini.
Na hivyo, akaomba kikao hicho kiahirishwe hadi pale Mahakama Kuu itakapoondoa marufuku hayo endapo itakubaliana na rufaa yake.
“Tayari nimekata rufaa dhidi ya amri iliyotolewa na Hakimu wa Mahakama ya Ufisadi iliyonizuia kuingia ofisini mwangu hadi kesi inayonikabili itakaposikizwa na kukamilishwa. Kwa hivyo, niko tayari kurejea hapa nikiwa na stakabadhi zote zitakazotoa majibu ya masuala yote yaliyoibuliwa kwenye ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali,” Bw Sonko akasema.
Profesa Ongeri alikubaliana na ombi hilo.
Baada ya kikao hicho, mwenyekiti huyo alimwalika Gavana Sonko kwa chakula cha mchana katika mkahawa wa majengo ya bunge.
“Mheshimiwa gavana utatuwia radhi hatukukupa chai. Lakini karibu, jumuika nasi kwa chakula cha mchana,” akasema Profesa Ongeri.
Sonko alirejea kwa kinasa sauti na kusema: “Mheshimiwa mwenyekiti niruhusu kuuliza hivi: Wapi baa; baa ya Senet?”
Aliuliza hivyo huku wanachama wengine wa CPAIC wakiangua kicheko.
Profesa Ongeri ambaye pia alicheka akajibu: “Hakuna baa katika Seneti mwaka huu kutokana na janga la Covid-19.”
Baada ya kupewa jibu hilo, Sonko aliondoka akiandamana na Afisa wa Masuala ya Sheria katika Kaunti ya Nairobi Lydia Kwamboka, msaidizi wake Ben Mulwa, Mkuu wa Wafanyakazi Brian Mugo na mshauri wa masuala ya kisheria Paul Musyimi.
Bw Sonko amewahi kuhudumu kama Seneta wa Nairobi kati ya 2013 hadi 2017 alipowania ugavana kwa tiketi ya Jubilee na kumbwaga Dkt Evans Kidero wa ODM.