Nia ya Raila yasalia kuwa siri kuu
Na VALENTINE OBARA
PENDEKEZO la Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, kuhusu marekebisho ya Katiba limezidi kuacha viongozi na wananchi wa pande zote za kisiasa wakijikuna vichwa kuhusu anachotaka kuafikia.
Sisitizo lake kuwa hana njama ya kujipangia mikakati ya 2022 kupitia muafaka huo halijazuia wanasiasa kuhisi ana nia fiche, huku wengine wakijaribu kutegua kitendawili chake.
Hali hii imezidishwa na jinsi wawili hao hawajatangaza lolote kuu kuhusu muafaka wao kufikia sasa, isipokuwa kuchagua kikundi cha watu 14 ambao pia majukumu yao hayajafafanuliwa wazi kwa umma.
“Inahitajika kuwe na ufafanuzi ili kuondoa usiri mkubwa ulio katika shughuli hii. Kwa sasa kuna hali ya kuchanganyikiwa kwani tayari kuna asasi za umma zinazofaa kushughulikia masuala yaliyotajwa kwenye muafaka wao,” alisema Katibu Mkuu wa Chama cha Amani National Congress, Bw Barrack Muluka.
Bw Odinga amependekeza kuwe na wadhifa wa waziri mkuu na manaibu wake, na kuwe na ngazi tatu za uongozi.
Mahasimu wake wanahofia kwa kupendekeza hivyo anatafuta mwanya wa kuingia serikalini kwa mlango wa nyuma na kufanya iwe vigumu kwa Naibu wa Rais William Ruto kuungwa mkono eneo la Kati mwaka wa 2022 na endapo Bw Ruto atashinda uchaguzini, asiwe rais mwenye mamlaka makubwa.
Mbunge wa Ndaragua, Bw Jeremiah Kioni, alisema ingawa Katiba inahitaji kurekebishwa, mbinu inayotumiwa ni ya kutiliwa shaka kwani inaonekana lengo ni kumvuruga Bw Ruto kisiasa.
“Jamii yetu iliahidi kumuunga mkono Bw Ruto. Huwezi kutufanya tuonekane tunamtoroka wakati huu. Tunahitaji marekebisho ya Katiba lakini mdahalo huu wote ulianzishwa kwa njia isiyofaa,” akasema Jumatatu.
Msimamo sawa na huu ulitolewa na wanasiasa wengine wa eneo la Kati ambao hawamwamini Bw Odinga.
Seneta wa Narok, Bw Ledama ole Kina ambaye ni mwanachama wa ODM, alikiri kuna hofu inayohitaji kutulizwa kabla watu wazungumzie marekebisho ya Katiba.
“Kwa kweli watu wana hofu. Hata mimi ningeogopa kama ningekuwa naibu wa rais kisha mtu aseme anataka kubadilisha katiba wakati nimekaribia kuingia mamlakani,” akasema.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Chama cha Third Way Alliance, Dkt Ekuru Aukot, alipendekeza katiba irekebishwe ili watu ambao wamewahi kuwa rais, naibu au makamu wa rais, waziri mkuu au naibu wasiruhusiwe kuwania urais.
Kulingana naye, hatua hii itafanya marekebisho yasilenge kutimiza maazimio ya wanasiasa ya kibinafsi, na itatoa nafasi kwa viongozi wapya kuongoza nchi.