Omar Lali aachiliwa
Na STEPHEN ODUOR
MAHAKAMA Kuu ya Garsen, Kaunti ya Tana River, Alhamisi ilimwachilia huru Omar Lali, mpenziye Bi Tecla Muigai, aliyepatikana amefariki mwezi Mei katika hali tatanishi.
Ilikuwa afueni kubwa kwa Bw Lali, aliyekabiliwa na shtaka la mauaji, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kuwasilisha shtaka hilo dhidi yake wiki moja iliyopita.
Lakini Alhamisi, Wakili wa Serikali Edie Kadebe, alisema kuwa upande wa mashtaka uliamua kusitisha shtaka hilo dhidi ya mshtakiwa, na badala yake kuanza kesi ya uchunguzi.
Alisema lengo kuu la uamuzi huo ni kuhakikisha kuwa kila upande umepata haki.
Marehemu ni mwanawe Bw Joseph Karanja na Bi Tabitha Karanja, ambao ndio wamiliki wa kampuni ya Kutengeneza Vileo ya Keroche mjini Naivasha.
“Ni suala ambalo tumelijadilia kwa kina. Tumetathmini kila mwelekeo tutakaochukua ambapo ili kuhakikisha kila upande umepata haki, tumeamua kuiendesha kesi hii kupitia uchunguzi wa mahakama,” akasema.
Jaji Roselyn Korir alikubai ombi hilo, na kumwachilia huru Bw Lali.
“Ikiwa itapatikana mshtakiwa ndiye alihusika, atakamatwa tena na kushtakiwa upya kulingana na maagizo yatakayotolewa,” akasema Jaji.
Mnamo Jumanne, mahakama iliagiza mshtakiwa kufanyiwa uchunguzi wa kiakili katika Hospitali ya Rufaa ya Garissa. Matokeo ya uchunguzi yalionyesha kuwa yuko katika hali nzuri kujibu shtaka dhidi yake.
Mshtakiwa alikamatwa na polisi kwa madai ya kushiriki mauaji ya marehemu.
Kulikuwa na ripoti kuwa wawili hao walikuwa na mzozo baina yao kabla marehemu kuanguka.
Hata hivyo, wakili wa marehemu alikanusha vikali madai hayo.
Makachero wanaochunguza tukio hilo walisema kuwa kulikuwa na hitilafu nyingi kwenye maelezo aliyotoa mshtakiwa kuhusu chanzo cha kifo cha marehemu.
Marehemu alifariki katika nyumba ya kibinafsi katika eneo la Shella, Kisiwa cha Lamu, baada ya kuanguka katika nyumba walimokuwa wakikaa pamoja na mshtakiwa.