Michezo

Real Madrid wapepeta Villareal na kunyanyua ubingwa wa La Liga

July 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

REAL Madrid walijitwalia ubingwa wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitatu huku wakisalia na mechi moja zaidi ya kusakata katika kampeni za msimu huu.

Hii ni baada ya kikosi hicho cha kocha Zinedine Zidane kuwapokeza Villarreal kichapo cha 2-1 ndani ya uwanja mtupu wa Alfredo Di Stefano mnamo Julai 16, 2020.

Real walipokezwa kombe la La Liga katika uwanja huo ulio na uwezo wa kubeba jumla ya mashabiki 6,000 pekee walioketi.

Kwa kawaida, uga huo hutumiwa na Real kufanyia mazoezi na wamechezea humo mechi zao zote za nyumbani tangu Juni 13 kwa kuwa uwanja wao mkuu wa Santiago Bernabeu unafanyiwa ukarabati.

Karim Benzema aliwaweka Real kifua mbele kunako dakika ya 29 baada ya kumzidi maarifa kipa Sergio Asenjo kisha kufunga bao la pili kupitia mkwaju wa penalti katika dakika ya 77.

Goli hilo la pili la Real lilihesabiwa baada ya penalti ya kwanza kufutiliwa mbali na refa kwa madai kwamba beki na nahodha Sergio Ramos alikuwa amegusa mpira kabla ya Benzema kuvurumisha fataki kimiani.

Ingawa Vicente Iborra alipania kuwarejesha Villarreal mchezoni kunako dakika ya 83, juhudi zake hazikutikisa uthabiti wa Real waliopania kutia kibindoni taji lao la 34 la La Liga na la kwanza tangu 2017. Real walishuka dimbani wakiwa tayari wametengenezewa jezi za kusherehekea ubingwa wa La Liga msimu huu. Jezi hizo ziliandikwa “Campeones 34” kwenye sehemu ya nyuma.

Chini ya Zidane ambaye ni mchezaji wa zamani wa Real, kikosi chake kimesajili ushindi kutokana na mechi zote 10 tangu kurejelewa kwa soka ya Uhispania mnamo Juni 13, 2020. Kivumbi cha La Liga kilikuwa kimesimamishwa kwa muda kutokana na janga la corona mnamo Machi 2020.

Real watashuka sasa ugani Municipal de Butarque kwa mchuano wa mwisho wa msimu huu dhidi ya Leganes wakijivunia pengo la alama saba kileleni mwa jedwali kuliko nambari mbili Barcelona.

Mataji ya La Liga yamekuwa machache sana kuliko yale ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) katika kabati la Real katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Ufalme wa msimu huu wa La Liga ni wa tatu kwa miamba hao kutia kapuni chini ya kipindi cha misimu tisa iliyopita. Hivyo, ufanisi wa Julai 16 uliwawezesha kukomesha kabisa ukiritimba wa Barcelona kwenye soka ya Uhispania.

Katika kipindi cha kwanza cha ukufunzi wa Zidane uwanjani Bernabeu, Real walinyanyua mataji matatu mfululizo ya UEFA huku wakiambulia nafasi ya tatu katika misimu yote hiyo kwenye La Liga.

Zidane ndiye aliyekuwa akidhibiti mikoba ya Real walipotwaa taji la La Liga mnamo 2017. Hata hivyo, aliagana rasmi na kikosi hicho mnamo 2018 na akarejea katikati ya msimu uliopita baada ya kusalia bila kikosi kwa takriban miezi saba.

Chombo cha Barcelona waliokuwa wakichezea uwanjani Camp Nou, kilizamishwa kwa mabao 2-1 na Osasuna ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya 11 jedwalini kwa alama 51 sawa na Athletic Bilbao.

Barcelona watafunga kampeni zao za La Liga msimu huu dhidi ya Alaves uwanjani Mendizorrotza mnamo Julai 19.

MATOKEO YA LA LIGA (Julai 16):

Barcelona 1-2 Osasuna

Real Madrid 2-1 Villarreal

Eibar 3-1 Real Valladolid

Athletic Bilbao 0-2 Leganes

Celta Vigo 2-3 Levante

Getafe 0-2 Atletico Madrid

Mallorca 1-2 Granada

Real Betis 1-2 Alaves

Real Sociedad 0-0 Sevilla

Valencia 1-0 Espanyol