TAHARIRI: Serikali iziokoe shule za wamiliki binafsi
Na MHARIRI
TANGU virusi vya corona kubainika nchini mnamo Machi, sekta nyingi muhimu ziliathirika, miongoni mwazo ikiwemo sekta ya elimu.
Kutokana na athari hizo, serikali ilichukua hatua za haraka kwa kutenga fedha kuzisaidia baadhi ya sekta kama sanaa, ambapo ilitoa Sh100 milioni kuwasaidia wanamuziki.
Makundi mengine katika jamii pia yamekuwa yakifaidika pakubwa, kutokana na mikakati ambayo imekuwa ikiendeshwa na viongozi mbalimbali kuyasaidia kukabili changamoto za kiuchumi.
Hata hivyo, wale ambao wamesahaulika kabisa ni walimu na hata wamiliki binafsi wa shule.
Kwa sasa, shule nyingi ziko katika hatari ya kufungwa kutokana na changamoto nyingi za kifedha zinazozikabili.
Kimsingi, shule hizo hutegemea karo inayolipwa na wanafunzi ili kuendesha shughuli zake, baadhi zikiwemo kuwalipa mishahara walimu.
Ikiwa dhahiri kuwa wanafunzi watarejea shuleni Januari mwaka ujao, walimu wengi wameeleza wasiwasi mkubwa kuhusu mustakabali wao.
Kumekuwa na ripoti nyingi zinazoonyesha kuwa kutokana na hali ngumu za kiuchumi, baadhi yao wamepatwa na maradhi yanayohusiana na mzongo wa mawazo.
Wengine wameripotiwa kujiingiza katika biashara, kilimo, uchukuzi kati ya shughuli zingine ili kujikimu kifedha.
Hata hivyo, kuna walimu ambao tegemeo lao kuu lilikuwa ni mishahara waliokuwa wakilipwa, hivyo hawakuwa wamejiwekea akiba yoyote.
Wengine wana familia ambazo zinawategemea kwa mahitaji yao ya kila siku kama chakula na kodi za nyumba. Hali ilivyo sasa, wengi hawajui watafanya nini. Wako katika njiapanda katika maisha yao.
Kulingana na takwimu, shule za wamiliki binafsi zimeaajiri zaidi ya wafanyakazi 200,000 kote nchini wanaowahudumia wanafunzi zaidi ya 300,000.
Hili ni kundi kubwa linalotoa mchango mkubwa kwenye ukuaji wa nchi.
Ikizingatiwa walimu walioajiriwa na serikali wanaendelea kupokea mishahara yao kama kawaida, ni wakati serikali iwakumbuke wenzao wa shule za wamiliki binafsi.
Mojawapo ya njia hizo ni kuzitengea shule hizo kiasi fulani cha fedha kuzisaidia kuhimili makali ya athari za virusi vya corona.
Hata ikiwa itazipa shule fedha hizo kama mikopo, itakuwa ishara nzuri kuonyesha kuwa inawajali wafanyakazi wake kama Wakenya wanaotoa mchango muhimu kwenye ukuaji wa nchi.