Habari Mseto

Washindi katika uchaguzi wa Alhamisi bungeni

July 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wa ODM, Wiper na Kanu na wale wa mrengo wa ‘Kieleweke’ katika Jubilee walitwaa nafasi za uongozi wa kamati za bunge katika chaguzi zilizofanyika Alhamisi.

Mbunge wa Kangema Muturi Kigano (Jubilee) alichaguliwa bila kupingwa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya kuhusu Haki na Masuala ya Kisheria (JLAC) huku Otiende Amollo (Rarieda, ODM) alipewa wadhifa wa naibu mwenyekiti.

Naye Mbunge wa Tiaty William Kamket (Kanu) ndiye mwenyekiti mpya wa Kamati ya Bunge kuhusu Sheria za Ziada, wadhifa ambao zamani ulishikiliwa na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Uasin Gishu Glady Boss Shollei. Naibu wake ni Mbunge wa Mbeere Kaskazini Bw Charles Muriuki Njagagua.

Kamati hizi mbili ndizo zitatwikwa wajibu wa kuandaa sheria zitakazofanikisha utekelezaji wa ripoti ya mpango wa maridhiano (BBI) na kuchanganua miswada ya marekebisho ya Katiba kupitia kura ya maamuzi. Hii ni ajenda kuu ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga

Naye Mbunge wa Moiben Silas Tiren alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo naye Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Laikipia Catherine Waruguru akachaguliwa kuwa naibu mwenyekiti.

Na kamati ya Leba sasa itaongozwa na Mbunge wa Limuru Peter Mwathi na Mbunge wa Chepalungu Gideon Kimutai (Chama cha Mashinani) ambao walichaguliwa bila kupingwa.

Mbunge wa Kieni Kanini Kega ambaye ni mkereketwa wa mrengo wa ‘Kieleweke’ leo Ijumaa atachaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, nafasi ambayo zamani ilishikiliwa na Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwa.

Bw Ichungwa ambaye ni miongoni mwa wabunge 16 wandani wa Naibu Rais William Ruto ambao waling’olewa kutoka uongozi wa kamati za bunge kwa madai ya kumkosea heshima Rais Uhuru Kenyatta, ameteuliwa kuwa mwanachama wa Kamati kuhusu Huduma za Wabunge.