Polisi watatu na mahabusu wawili Thika wapatikana kuugua Covid-19
Na LAWRENCE ONGARO
UGONJWA wa Covid-19 unazidi kusambaa kote nchini na maafisa wa polisi na mahabusu kadhaa Kaunti ya Kiambu ni miongoni mwa walioambukizwa.
Kamanda wa polisi Kaunti ya Kiambu, Bw Ali Nuno, amesema kwamba maafisa watatu na mahabusu wawili walithibitishwa kuwa na homa ya corona.
Alisema Alhamisi kwamba kati ya mahabusu 70 waliokuwa rumande ya kituo cha Thika, wawili walithibitishwa kuambukizwa corona.
“Baada ya maafisa wa afya kuthibitisha hayo tayari mahabusu wapatao 68 wamepimwa corona huku wakingoja kupata matokeo yao. Wakati huo pia maafisa wa polisi 25 katika kituo cha Thika wamepimwa pia na wanasubiri matokeo,” alisema Bw Nuno.
Alisema mahabusu wapya watapelekwa sehemu za Ngoliba, Thika Mashariki.
“Tutafanya juhudi kuona ya kwamba mahabusu walioko katika kituo cha Thika mjini hawajumuiki na mtu yeyote. Tunataka kuweka tahadhari kwa kila mwananchi,” alisema Bw Nuno.
Aliyasema hayo alipozuru kituo cha polisi cha Thika kutathmini hali ilivyo.
Alisema kwa wakati huu, wamesitisha mahabusu kupelekwa katika seli ya kituo hicho kutokana na jambo hilo.
“Tayari tumetoa wito kwa maafisa wetu wawe makini wanapotangamana na watu wanaofika katika kituo. Ni sharti kila mmoja anawe mikono, avalie barakoa na kuweka nafasi ya mita moja au zaidi kutoka pahala aliko hadi kwa mwingine.
Alisema afisa yeyote wa polisi atakayepatikana na virusi vya corona atapelekwa katika hospitali ya Tigoni Level 4, Limuru, ambayo imetengwa kwa ajili ya wagonjwa wa Covid-19.
“Kwa wakati huu kila mmoja ni lazima ajichunge mwenyewe ili tuweze kukabiliana na janga hili la corona,” alisema Bw Nuno.
Alisema maafisa wa polisi wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa bila kutarajia kutokana na wao kuwa katika kazi inayofanya iwe rahisi kuwa palipo na watu wengi kila wakati.