• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Mjiandae kusoma ‘Siku Njema’ kwa lugha ya Kichina

Mjiandae kusoma ‘Siku Njema’ kwa lugha ya Kichina

Na CHARLES WASONGA

RIWAYA ya ‘Siku Njema’ sasa itatafsiriwa kwa lugha ya Kichina kama ishara ya heshima kwa mwendazake Prof Ken Walibora.

Mchakato huo wa tafsiri utafanywa na Mchina Yuning Sheng ambaye ni Msomi wa Kiswahili na Isimu ya Afrika alifanya tafiti nyingi kuhusu fasihi ya Afrika Mashariki alipokuwa akisoma nchini Ujerumani.

Mradi huo utafadhiliwa na Taasisi ya China Academy of Social Sciences (CASS) kama sehemu ya mpango wake wa kuvumisha kazi za marehemu Walibora nchini China.

“Miezi michache iliyopita msomi kutoka taasisi ya CASS aliniuliza nitafsiri riwaya ya ‘Siku Njema’ kwa lugha ya Kichina na nikakubali kujiendesha kibarua hicho.

“Isitoshe, nina nakala ya tafsiri ya Kiingereza, ‘A Good Day’ ambayo marehemu Walibora alinipa kama zawadi tulipokutana katika kongamano fulani,” Sheng akasema kwenye makala yake yaliyochapishwa katikaSaturday Nation toleo la Julai 18, 2020.

Alihimiza kwamba zaidi ya vitabu 40 vya riwaya na hadithi fupi vilivyoandikwa na mwandishi huyo mashuhuri zitumike kote ulimwenguni kwani ni kazi zilizosheheni utajiri mkubwa wa fasihi ya Afrika Mashariki,” akaongeza.

Riwaya ya ‘Siku Njema’ iliteuliwa kama kazi ya kutahiniwa katika shule za upili kati ya miaka ya 1997 na 2003.

Ni mojawapo kati ya kazi mufti za Walibora. Katika riwaya hiyo marehemu Walibora anasimulia kuhusu maisha ya kijana mmoja utotoni nyumbani kwao Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia.

Walibora alifariki mnamo Aprili 10 baada ya kuhusika katika ajali katika barabara ya Landhies, Nairobi.

Kazi zake zingine ni ‘Ndoto ya Amerika’ na ‘Kidagaa Kimemwozea’ kilichotumiwa kufunzia fasihi katika shule za upili nchini mnamo 2013.

Vilevile aliandika ‘Kufa Kuzikana’, ‘Ndoto ya Almasi’, ‘Mbaya Wetu’, na ‘Damu Nyeusi’ ambacho alihariri pamoja na Said A. Mohamed.

You can share this post!

COVID-19: Kenya yathibitisha visa 688 vipya ikiwa idadi ya...

Barcelona katika hatari ya kuwa ‘AC Milan au...

adminleo